Rais Paul Kagame wa Rwanda amewataka viongozi wa Afrika kuitumia dhana ya Akili Mnemba(AI) ili kuhakikisha kuwa bara hilo halibaki nyuma katika mapinduzi ya kiiteknolojia.
Akizungumza wakati wa Kongamano la Akili Mnemba barani Afrika, jijini Kigali siku ya Aprili 3, Rais Kagame alisema kuwa ipo haja kubwa ya kufanya uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya kidijiti, maendeleo ya rasilimali watu na mtangamano wa bara zima la Afrika ili kuhakikisha kuwa bara hilo linapata faida za Akili Mnemba.
“Afrika haiwezi kubaki nyuma. Ni lazima tukubali kushirikiana na kushindana kwa maslahi yetu mapana. Na ndio maana tupo hapa,” alisema.
Kongamano hilo la siku mbili, limewaleta pamoja zaidi ya watunga sera 1,000, wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika sekta ya teknolojia na ubunifu.
Katika hatua nyingine, Kagame aliupongeza Umoja wa Afrika, Baraza la Shirika la Mawasiliano duniani (ITU) na Smart Afrika kwa kuchochea kuanzishwa kwa baraza la Akili Mnemba barani Afrika.
“Bara letu lina uwezo na ubunifu wa hali ya juu ambao ni faida kwetu. Kwa sasa, kipaumbele chetu kiwe kujenga msingi imara wa kuunganisha mitandao,” aliongeza.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Google mwaka jana, teknolojia ya Akili Mnemba itaongeza Dola Bilioni 30 kwenye uchumi wa kusini mwa jangwa la Sahara.