Wizara ya Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii nchini Uganda imekabidhi rasmi magari mapya kwa viongozi wa kitamaduni waliotangazwa kwenye gazeti la serikali ili kuwawezesha katika kuhamasisha jamii zao kwa ajili ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Serikali ya Uganda inatambua falme za Buganda, Bunyoro-Kitara, Toro na Acholi.
Mbali na hizo, kuna kabila nyengine ambazo zina machifu ambao serikali imeweka katika mipango yake ya uonozi wa kitamaduni.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Aggrey Kibenge alibainisha kuwa utoaji wa magari hayo unaonyesha heshima kubwa ya serikali kwa urithi wa kitamaduni na mila za Uganda.
"Taasisi za kitamaduni kwa muda mrefu zimekuwa msingi wa mwongozo wa maadili, utatuzi wa migogoro, na uhifadhi wa kitamaduni, ”Kibenge alisema.
“Wakati Uganda inaendelea kwenye njia yake ya maendeleo, taasisi hizi zinasalia kuwa washirika muhimu katika kukuza amani, utambulisho wa kitamaduni, na uhamasishaji wa jamii kwa ajili ya mabadiliko," aliongezea.
Lakini zawadi hizi zinatolewa huku nchi hiyo ikiwa tayari katika kampeni ya Uchaguzi Mkuu unaofaa kufanyika Januari 2026. Rais Yoweri Museveni anagombea kiti tena na kama historia inavyoonyesha amewatumia viongozi wa kitamaduni kuhamasisha kura kwa wafuasi wao katika kampeni za mihula iliyopita.