Sudan Kusini imetimiza miaka 14 tangu uhuru wake huku rasilimali ya mafuta nchini humo ikiendelea kuwa tegemeo kubwa la nchi hiyo.
Baada ya kupata uhuru mwaka Julai 2011 kutoka Sudan, Sudan Kusini ilirithi takriban asilimia 75 ya uzalishaji wa mapipa ya mfuta 470,000 kwa siku ambayo ilikuwa ikifanyika Sudan kwa jumla.
Lakini nchi hiyo changa zaidi duniani, imejikuta bado haina miundombinu ya usafirishaji wa mafuta ghafi, hivyo mafuta yake lazima yapitie Sudan yenye bandari kwa ajili ya mauzo ya nje.
Sekta ya mafuta ndiyo kichocheo kikuu cha uchumi wa nchi hiyo ikichangia takriban asilimia 60 ya Pato la Taifa, wakati mapato yanayohusiana na mafuta yanachukua kati ya asilimia 90 ya mapato ya serikali.
Hata hivyo, haijavuna ipasavyo kutokana na utajiri huu kwani miaka miwili tu baada ya uhuru, kuliibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisambaratisha umoja wa serikali ya mpito ambao ulitakiwa kuiongoza nchi hiyo kufikia uchaguzi mkuu.
Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa Machi 2025 inaonyesha kuwa kufikia mwaka 2023 Sudan Kusini ilikuwa inazalisha mapipa 139,000 kwa siku.
Hata hivyo, kiwango hicho kilipungua mwaka uliofuata na kufikia mapipa 120,000.
Mwaka huu 2025 Sudan Kusini inazalisha takriban mapipa 66,000 tu kwa siku. Uzalishaji wa utajiri huu unaathiriwa na sababu tofauti.
Moja ya makampuni mkubwa ya uzalishaji wa mafuta nchini Sudan Kusini, Shirika la Kimataifa la Petronas, lilitangaza kuondoka rasmi nchini humo mnamo Agosti 2024.
Hii iialithiri uwezo wa nchi hiyo kuzalisha zaidi ya mapipa 155,000 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kupasuka kwa bomba la mafuta nchini Sudan mwaka 2024, ambalo linatumika kusafiriksha theluthi mbili ya mafuta ya Sudan Kusini kufikia Bandari ya Sudan, kuliliingiza taifa hilo changa katika mdororo wa kiuchumi.
Bila kusahau uwepo wa vita katika nchi jirani ya Sudan tangu Aprili 2023.
Hata kabla ya mshtuko huu uchumi wa Sudan Kusini ulikuwa chini ya kiwango kutokana na miaka ya mfululizo ya mafuriko makubwa. Athari za vita vya Urusi na Ukraine na athari za Uviko 19, zimechangia uwekezaji na uzalishaji duni wa mafuta.
Lakini kikubwa zaidi ni shida ya ndani ya nchi. Mvutano wa kisiasa uliozua vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, bado haujaruhusu nchi hiyo kuwa na utulivu kwa takriban raia milioni 11 waliokuwa na matumaini makubwa pindi nchi hiyo ilipojipatia uhuru mwaka 2011.