Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameshtumu vikali hatua za Israeli katika Haram al Sharif, akisisitiza kuwa Msikiti wa Al Aqsa na maeneo yake ya karibu ni ya Waislamu pekee na yaachwe kama yalivyo.
“Haram al Sharif, ambapo ni pamoja na Msikiti wa Al Aqsa na Qubbet al Sakhra, ni sehemu moja ya ardhi ambayo haitakiwi kugawanywa, na eneo lote la ekari 144, ni la Waislamu pekee,” Erdogan alisema wakati wa hotuba yake jijini Istanbul siku ya Ijumaa katika mkutano wa 3 wa Kimataifa wa Yeditepe unaofanyika kila baada ya miaka miwili.
“Hatutaruhusu mtu kufanya dharau na hili.”
Alisema kuwa kuingia Al Aqsa ni “kuvuka mpaka” kwa Uturuki, akisisitiza kuwa daima itakuwa hivyo. Erdogan alitaka Israeli iache uchochezi wa aina yoyote, uvamizi, na mambo ambayo yanatishia utukufu na umoja wa eneo hilo tukufu.
“Uturuki haijawahi kunyamazia ukandamizaji na vurugu katika kanda yetu. Hatutanyamaza sasa,” aliongeza, akisisitiza kuwa ataendelea kuunga mkono haki za msingi za Palestina na kutetea maeneo matakatifu ya Waislamu.
‘Kutetea Palestina ni kutetea ubinadamu, haki, na amani’
Mapema siku ya Ijumaa, Erdogan alishtumu tena mashambulizi ya Israeli katika vita vinavyoendelea Gaza, akitaja kukaa kimya kwa ulimwengu kuhusu ukatili unaoendelea ni kama “kuvunjika kwa maadili” na kusisitiza kuwa Uturuki inawaunga mkono watu wa Palestina bila shaka yoyote.
"Kutetea suala la Palestina siyo tu kusimama na watu wanaoteswa," Erdogan alisema Ijumaa wakati wa mkutano wa wawakilishi wa mabunge yanayounga mkono Palestina jijini Istanbul, Uturuki.
"Ni kuhusu kutetea ubinadamu, amani, na haki," alisema.
Tangu Oktoba 7, 2023, Wapalestina zaidi ya 51,000 wameuawa na mashambulizi ya Israeli huko Gaza, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.
Erdogan alielezea mashambulizi haya kama “mihemko ya machafuko,” akishtumu serikali ya Israeli kwa kuwaua raia — ikiwemo watoto, wanawake, wazee, na hata watoto wachanga.
"Waandishi wa habari wanauawa huku vyombo vya habari vya kimataifa vikikaa kimya. Watoto wanauawa kikatili huku watetezi wa haki za binadamu wakikaa kimya," alisema.
‘Mataifa ya Magharibi yanajifanya hayaoni’
Erdogan ameshtumu mataifa ya Magharibi kwa kile alichokiita unafiki wa kutochukua hatua.
"Wale ambao wamekuwa wakijisifu kuhusu kuheshimu uhuru, haki, sheria, na uhuru wa habari wanajifanya hawaoni yanayotokea kwa miezi 18 huku Israeli ikiendeleza sera ya ukatili ," alisema.
Alihoji kuhusu undumakuwili wa nchi ambazo mara moja kuwekea watu wengine vikwazo lakini sasa wako kimya kuhusu mzozo huu: "Mataifa ya Magharibi, ambayo hutumia silaha ya vikwazo hata kwa mambo madogo, nawauliza — mko wapi sasa linapokuja suala la Israeli?"
‘Utaratibu wa dunia ambao unapuuza wanaoteswa wanakuwa chini ya amri ya wanaotesa’
“Utaratibu wa dunia ambao hausimami na watu wanaoteswa inakuwa ni fursa kwa watesaji ,” Erdogan alionya, akiangazia kushindwa kwa taasisi za kimataifa kutaka uwajibikaji kuhusu Gaza.
Pia alieleza kusikitishwa sana na mataifa ya Kiislamu: "Inaniuma sana kusema hivi — na moyo wangu unavuja damu — lakini mataifa ya Kiislamu yameshindwa kutekeleza wajibu wake."
‘Waandishi wa habari wanauawa, familia zinasambaratishwa’
Kufikia Aprili 2024, waandishi wa habari wasiopungua 212 na wafanyakazi wa mashirika ya habari wameuawa Gaza tangu kuanza kwa mapigano, kufanya iwe ni kipindi kibaya zaidi kwa waandishi wa habari katika historia ya sasa, kulingana na rais wa Uturuki.
“Siku chache tu zilizopita,” Erdogan amesema, “mwandishi wa kike alikufa shahidi pamoja na watu 10 wengine wa familia yake — kuuawa kwa kutoa taarifa za ukweli.”
Alilalamika kuhusu hali ya sheria ya kimataifa: “Haiangalii haki tena. Imekuwa ni sehemu ya kuimarisha nguvu ya wenye uwezo.”
Njaa kutumika kama silaha, mapambano ya kujilinda kuitwa ugaidi’
Israeli imezuia kabisa misaada kuingia Gaza, kusababisha Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kuonya kuhusu njaa kali eneo hilo. Erdoğan amelaumu Israeli kwa kutumia njaa kama silaha: “Kwa wale ambao hawawezi kuwaua kwa mabomu, wanawanyima chakula, maji, na dawa. Ni mfumo mahsusi wa kuwaangamiza.”
Alilaani kitendo cha kuita mapambano ya kujitetea ya Wapalestina ugaidi: "Wale ambao walikuwa kimya wakati Wapalestina wakiuawa kikatili sasa wanaita mapambano ya kujitetea Gaza ugaidi — kujaribu kushabikia mauaji ya halaiki."
‘Mashariki ya Kati inawaka moto, dunia iko hatarini’
Erdoğan pia ameshtumu Israeli kuendeleza mapigano ya kijeshi ikilenga Syria na Lebanon, akionya kuwa kuongezeka kwa hali hii kutaingiza kanda nzima katika vita.
“Mashambulizi nchini Syria na Lebanon yanadhihirisha kuwa serikali ya Netanyahu haitaki amani au utulivi Mashariki ya Kati.”
"Huu uwendawazimu, ambao unatishia na kufanya hali kuwa tete kwenye kanda nzima, lazima uishe mara moja," alisema. "La sivyo, huu moto utawameza wale ambao wanauchochea."
‘Tutasimama na Palestina, hata tukiwa peke yetu’
Erdogan amekataa mapendekezo yanayolenga kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao ya kihistoria: "Kwa vyovyote vile inavyosemekana, kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao ambayo wameishi kwa maelfu ya miaka hakuna msingi wowote kwetu sisi."
Uturuki, alisisitiza, haitorudi nyuma kwa hilo: "Tutafanya kila tuwezalo kuwasaidia Wapalestina waishi kwa uhuru katika ardhi yao. Hata kama tutakuwa peke yetu, tutaendelea kuwatetea Wapalestina."