Hizi ni baadhi ya dalili kwamba umemvutia, lakini anakusubiri uchukue hatua
Hizi ni baadhi ya dalili kwamba umemvutia, lakini anakusubiri uchukue hatua
Katika maisha ya kawaida, ni jambo la kawaida kwa watu wa jinsia mbili tofauti kujikuta wamevutiwa. Hii inaweza kutoka mahali popote ikiwemo mtaani unapoishi au hata sehemu ya kazi.
11 Julai 2025

Katika maisha ya kawaida, ni jambo la kawaida kwa watu wa jinsia mbili tofauti kujikuta wamevutiwa. Hii inaweza kutokea mahali popote ikiwemo mtaani unapoishi au hata sehemu ya kazi.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa, baadhi wanashindwa kuchukua hatua yoyote kwa sababu ya kutotambua dalili za kuvutiwa.

Katika hatua hii, tahadhari na umakini unahitajika hasa kwa mwanamume, kwa sababu, ni wanawake wachache mno, wenye ujasiri wa kusema au kuelezea hisia zao. Sio kwa sababu hawataki kusema, bali nao wanasubiri kwa matumaini kwamba mwanamme atakuwa wa kwanza kuchukua hatua.

Hii inaweza kuwa ni kutokana na aibu, lakini pia kuna hofu ya kukataliwa.  Zaidi ya yote, jinsi mfumo wa jamii ulivyojengeka hasa linapokuja suala la mahusiano na nani anatakiwa kuanza. Kwa maana hiyo, bila kusema, wanawake mara nyingi huonyesha dalili zifuatazo:

1. Anajitokeza au kujipitisha mara kwa mara sehemu ulipo. Unaweza kushangaa, kila unapokwenda pengine katika mghahawa, unakutana nae. Hii ni kwa sababu pengine, amejua muda wake, hivyo na yeye anajisogeza karibu muda huo ili umuone.

2. Anatafuta sababu ya kuwa karibu na wewe. Kama ni katika mazingira ya kazi, anaweza kuja kwako mara kwa mara, pengine kuuliza kitu, au kutaka msaada wa kikazi.

3. Vitendo vyako vinafanana na vyake. Kwa mfano, mnapokuwa pamoja, ukikunja miguu, na yeye bila kujua, utakuta amekunja miguu, ukisogea karibu, na yeye anaweza kufanya hivyo hivyo.

4. Anauliza maswali zaidi ya mazungumzo ya kawaida. Kwa namna moja au nyengine, utagundua kwamba, katika mazungumzo yenu, anapenda kuuliza maswali yanayohusu maisha binafsi zaidi. Labda unapendelea kula nini, unapenda kufanya nini wakazi wa mapumziko, na hali kadhalika.

5. Anakusifu kwa njia ambayo sio ya moja kwa moja. Anaweza asikuambie kwamba umependeza, lakini anaweza kukuambia kwamba shati ulilolivaa ni zuri. Au, unapendeza ukivaa nguo ya rangi fulani.

6. Anachangamka unapokuwa karibu. Unaweza kushangaa, unatokea tu, anaweza kuacha alichokuwa anafanya, na kukupa muda wake. Muangalie usoni, bila shaka utaona jinsi uso wake na macho yake yalivyochangamka.

7. Anakumbuka vitu vidogo vidogo katika mazungumzo yenu. Mathalan, anaweza kukumbuka kwamba ulimuambia unapenda kula aina fulani ya chakula. Pia anaweza kukumbuka siku yako ya kuzaliwa.

8. Anaweza pia kuonyesha dalili za kuwa na wasiwasi hasa unapokuwa karibu, hii inaweza isiwe kwa ubaya. Kwa mfano, anaweza kuchezea bangili yake, au kucheka sana bila sababu.

9. Anakupa nafasi ya kukutana nae tena na tena. Kwa mfano, anaweza kukuambia, napenda kwenda katika mghahawa fulani, au tujaribu kwenda eneo fulani. Hizi ni dalili za mualiko, ingawa sio moja kwa moja. Hivyo, kama na wewe umevutiwa, basi unaweza kutumia fursa hiyo kumualika kupata kikombe cha kahawa sehemu au chakula cha usiku.

Kumbuka, jamii ina mtizamo tofauti katika suala zima la mahusiano. Mara nyingi, imezoeleka kwamba, ni mwanamume ndie mwenye kuanza, lakini bila kuona baadhi ya dalili, nae pia inaweza kumuia vigumu kuchukua hatua.

 

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us