Afrika Kusini imeshtumu mashambulizi ya mabomu ya Israeli dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza, kufuatia mashambulizi ya makombora wiki iliyopita katika hospitali ya Al-Ahri Arab kwenye eneo hilo.
“Afrika Kusini inajiunga na dunia katika kushtumu mashambulizi ya mabomu, ambapo ni wazi kuwa wanakiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu,” Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa siku ya Jumatano.
Ilisema kuwa Israeli imeshambulia kwa mabomu, kuchoma na kuharibu hospitali zisizopungua 35 Gaza tangu Oktoba 2023.
“Mashambulizi katika vituo vya afya, kuwashambulia wahudumu wa afya na wagonjwa inakuwa ni uhalifu wa kivita kwa mujibu wa makubaliano ya IV ya Geneva ya mwaka 1949,” ilisema taarifa.
Kushambulia wahudumu wa afya
Ikiangazia mauaji ya wahudumu 15 wa afya na wale wanaotoa usaidizi Gaza, ambao “walishambuliwa kwa makusudi” na wanajeshi wa Israeli wakati wakijaribu kuokoa watu, ilisema: “Mashambulizi ya makusudi kwa wahudumu wa afya na wafanyakazi wa mashirika ya misaada hayaruhusiwi kulingana na sheria ya kimataifa na inakuwa ni uhalifu wa kivita.”
“Maafisa wa kutoa misaada ya dharura kama raia na wengine ambao si wapiganaji hawatakiwi kulengwa,” iliongeza.
Ikieleza kuhusu wasiwasi wake kwa Israeli kuzuia misaada kuingia Gaza tangu 2 Machi, ilisema: “Huku ni kukiuka maagizo ya muda ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo iliitaka Israeli kuruhusu misaada kuingia Gaza bila vizuizi vyovyote.”
Wizara hiyo ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha Israeli kwa kuchukua “hatua kali, kutokana kuwa kuachiwa kwa Israeli kufanya wanavyotaka kumewapa nguvu ya kuendeleza mauaji ya halaiki Palestina.”
Kesi ya ICJ
Baada ya Afrika Kusini kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israeli kwa kukiuka makubaliano ya Geneva ya 1948 ya mauaji ya halaiki huko Gaza, nchi kadhaa zilijiunga kwenye kesi hiyo ikiwemo Colombia, Cuba, Libya, Mexico, Hispania, Belize, na Uturuki.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) pia ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu Gaza.
Rais wa Marekani Donald Trump ameiwekea vikwazo ICC kwa kufanya uchunguzi dhidi ya maafisa wa Israeli.