AFRIKA
3 dk kusoma
UN yasikitishwa na mauaji wakati wa maandamano ya 'Saba Saba' Kenya
Jeshi la Polisi nchini Kenya, limeripoti kwamba watu 11 wanahofiwa kupoteza maisha wakati wa maandamano hayo, huku polisi 52 wakijeruhiwa na wengine 567 wakishikiliwa na polisi.
UN yasikitishwa na mauaji wakati wa maandamano ya 'Saba Saba' Kenya
Polisi waliweka ulinzi mkali jijini Nairobi siku ya 'saba saba' / picha: AP
8 Julai 2025

Umoja wa Mataifa umesikitishwa na taarifa za mauaji ya watu wakati wa maadhimisho ya ‘Saba Saba’, yaliyofanyika nchini Kenya, Julai 7, 2025.

“Tumesikitishwa sana na mauaji yaliyotokea jana pamoja na uporaji na uharibifu wa mali nchini Kenya wakati polisi na vikosi vingine vya usalama vikikabiliana na waandamanaji jijini Nairobi na kaunti zingine 16,” alisema Ravina Shamdasani, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu katika ripoti yake.

“Mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za kawaida na zile za mpira zilitumika,” alisema ofisa huyo wa Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Kenya iliimarisha ulinzi mkali katika jiji la Nairobi na maeneo mengine ili kuweza kuwadhibiti waandamanaji siku ya ‘Saba Saba.

Ilikuwa ni vigumu kuingia na kutoka jijini Nairobi baada ya kufungwa kwa barabara muhimu huku shule zikifungwa kwa kuhofia usalama wa wanafunzi.

Jeshi la Polisi nchini Kenya, limeripoti kwamba watu 11 wanahofiwa kupoteza maisha wakati wa maandamano hayo, huku polisi 52 wakijeruhiwa na wengine 567 wakishikiliwa na polisi.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya iliripoti jumla ya vifo 10 na majeruhi 29, huku watu 37 wakishikiliwa na polisi.

“ Tumepokea ripoti za uporaji na uharibifu wa mali ya umma na zile za binafsi. Inasikitisha sana kwamba matukio ya hivi karibuni yanatokea wiki mbili baada ya waandamanaji 15 kuripotiwa kuuwawa na wengine kujeruhiwa jijini Nairobi na maeneo mengine ya Kenya,” aliongeza msemaji huyo.

“Tunatambua kuwa polisi wametangaza uchunguzi wa matukio ya awali. Kamishna Mkuu anarudia rai yake dhidi ya mauaji yote yaliyoripotiwa na madai mengine ukiukwaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhusu matumizi ya nguvu, kuchunguzwa kwa haraka, kwa kina na kwa uwazi. Waliohusika lazima wawajibishwe,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen amewashukuru na kuwapongeza maofisa polisi nchini humo kwa ‘kazi nzuri’.

“Shukrani kwa juhudi zao na maafisa wengine kote nchini, visa vya ghasia, uporaji na uharibifu wa mali vimepungua leo ikilinganishwa na wiki iliyopita. Tumejitolea kuhakikisha kuwa maandamano yanafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Murkomen wakati akizungumza na maofisa polisi Jumatatu jioni, jijini Nairobi

Wakati huo huo Waziri huyo amekosolewa na baadhi ya baadhi ya watetezi wa haki za binadamu, wakidai kuwa yeye ndiye chanzo cha raia kuuwawa.

“Tunasema Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen awajibike kwa matukio ya watu kupigwa risasi wakati wa maandamano ya Saba Saba. Vitendo hivi vinafanyika kwa ufahamu kamili wa mamlaka, hasa baada ya yeye (Murkomen) kuwapa polisi amri ya 'kupiga risasi na kuua,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Vocal Africa, Hussein Khalid.

CHANZO:TRT Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us