Katika miaka ya hivi karibuni, masuala ya Afrika yamekuwa yakipewa nafasi ya kipekee katika majukwaa ya kimataifa, na hali hii imejidhihirisha kupitia Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya, ambalo limekuwa likiwakutanisha viongozi wa kimataifa, wanadiplomasia, na watunga sera kutoka pembe zote za dunia.
Makala ya mwaka huu ya kongamano, halikugusia tu muktadha wa siasa na machafuko yanayoendelea ndani ya bara hilo, bali pia liliangazia nyanja za utamaduni na maendeleo ya jamii, hasa kwa wanawake.
Mojawapo ya vielelezo nafasi ya Uturuki katika kukuza ushirikiano na bara hilo lenye rasilimali lukuki ni uwepo wa Jumba la Utamaduni wa Afrika (African House Culture), taasisi iliyoanzishwa mwaka 2016 kwa juhudi za dhati za Mke wa Rais wa Uturuki, Bi Emine Erdoğan.
Kupitia taasisi hii, jumba la utamaduni limejenga daraja la kitamaduni linalounganisha mataifa ya Afrika na wananchi wa Uturuki kwa njia ya kuhifadhi, kutangaza, na kuthamini utajiri wa kazi za mikono kutoka mataifa ya Afrika.
Bi Emine Erdoğan, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii zilizo pembezoni, hasa wanawake na wajasiriamali wadogo barani Afrika, ameonesha dhamira yake kupitia ziara nyingi katika nchi za Afrika.
Akiwa ameandamana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan katika safari hizo, amekuwa akishuhudia changamoto zinazowakabili wanawake, wengi wao wakiwa na vipaji na ujuzi wa kutengeneza bidhaa za kipekee, lakini wakikumbwa na matatizo ya upatikanaji wa masoko ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Bi Zeliha Saglam, Mkuu wa Jumba la Utamaduni wa Afrika, juhudi za Emine Erdoğan ziliibua wazo la kuanzisha taasisi hiyo kama jukwaa la kuonesha kazi za mikono kutoka Afrika.
“Mke wa Rais alipokuwa akiambatana na mumewe katika safari nyingi barani Afrika, aliona kuwa wanawake wanatengeneza vitu vya thamani lakini hawapati fursa za masoko. Ndipo wazo la kuanzisha jumba hili likazaliwa, kwa lengo la kusaidia wanawake hao,” alisema Saglam.
Katika Kongamano la mwaka huu, jumba hilo liliwasilisha baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa kwa mikono kutoka zaidi ya nchi 40 za Afrika. Hizi ni bidhaa ambazo si tu zinaonesha ubunifu na ustadi wa watengenezaji wake, bali pia ni vielelezo vya urithi wa kitamaduni wa jamii zao.
“Hivi unavyoviona hapa ni baadhi tu ya kazi za mikono zilizotengenezwa na wanawake kutoka nchi mbalimbali, na zimewekwa hapa ili zitambulike na kuthaminiwa kimataifa,” aliongeza Bi Saglam, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Alionesha kwa mfano begi lililotengenezwa na mwanamke mwenye ulemavu kutoka Senegal, akieleza kuwa walilinunua kwa lengo la kusaidia jamii ya watu wenye ulemavu katika nchi hiyo.
Upo pia mkufu uliotengenezwa kwa kutumia shanga, kutoka Tanzania, kama ishara nyingine ya mchango wa wanawake wa Kiafrika katika sekta ya urembo wa jadi.
"Tumenunua vitu vingi kutoka zaidi ya nchi 40 za Afrika na kuzileta hapa ili kuwasaidia jamii, haswa wanawake na walemavu,” alisema Saglam, akisisitiza dhamira ya kituo hicho katika kupaza sauti za wasio na sauti kupitia utamaduni.
Jumba la Utamaduni wa Afrika limekuwa likiwakutanisha wadau mbalimbali kama wanadiplomasia, watunga sera, wafanyabiashara na wanafunzi, kwa madhumuni ya kukuza ushirikiano wa kiutamaduni kati ya Afrika na Uturuki.
Mikutano na majukwaa kama Kongamano la Diplomasia la Antalya yamekuwa nyenzo muhimu ya kukuza uhusiano huu kwa njia yenye tija na ushawishi mkubwa.
Kwa kuzingatia umuhimu wa utamaduni kama nyenzo ya diplomasia, ushirikiano huu unatoa mwanya mpana kwa wanawake wa Kiafrika kujiinua kiuchumi, kijamii, na kimataifa.
Na kwa juhudi kama hizi, Afrika inazidi kuthaminiwa si tu kwa rasilimali zake, bali pia kwa hazina yake ya kipekee ya tamaduni.