Washika bunduki wa London wanaingia katika uwanja wa Santiago Bernabeu wakiwa na magoli matatu kibindoni, jambo ambalo linawapa matumaini kiasi.
Real Madrid, ambao ni mabingwa mara 15 wa UEFA, wamejinasibu kupindua matokeo hayo, na kusonga mbele kwenye michuano hiyo, ambayo wanayaita ‘ya kwao’.Je, watafanikiwa kufanya miujiza ndani ya uwanja wao wa nyumbani usiku wa leo?
Ndiyo mabingwa watetezi na wanafahamu vizuri maana ya kuwa katika hatua hii.
Katika mashindano haya tangu kupewa jina lake la sasa mwaka 1992 timu nne pekee zimefanikiwa kupindua matokeo ya magoli matatu au zaidi. Arsenal wako kwenye nafasi ya kuweka historia ya kuingia nusu fainali ya ligi hiyo tangu 2009.
Katika historia Real Madrid haijawahi kuifunga Arsenal. Timu hizo zimekabiliana mara tatu ikiwemo wiki iliyopita.
Arsenal imepata ushindi katika mechi mbili, na kutoka sare kwenye mechi moja. Mechi mbili zingine ambazo timu hizi zimepambana ilikuwa kwenye hatua ya 16 msimu wa 2005-06 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambao ndiyo msimu pekee kwa Arsenal kucheza fainali ya mashindano haya na walifungwa na timu nyingine ya Hispania, Barcelona.