AFRIKA
2 dk kusoma
Watu 35 wauawa nchini Sudan kutokana na mashambulizi ya RSF El-Fasher: Jeshi
Jeshi linasema limefanikiwa kukabiliana na mashambulizi ya wapiganaji wa RSF, na kuwaua 80, pamoja na kuharibu magari yao 10
Watu 35 wauawa nchini Sudan kutokana na mashambulizi ya RSF El-Fasher: Jeshi
18 Aprili 2025

Raia wasiopungua 35 wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa baada ya wapiganaji wa RSF kushambulia mitaa yao katika mji wa El-Fasher, Kaskazini mwa Darfur, jeshi la Sudan lilisema siku ya Ijumaa.

Katika taarifa, kikosi cha jeshi kilichoko eneo la El-Fasher kilisema RSF “ilishambulia kwa makombora” siku ya Alhamisi, ikilenga maeneo kadhaa katika mji huo.

Kulingana na jeshi, mashambulizi hayo, yaliwaua watu 35, ikiwemo wanawake, watoto, na wazee, 40 wakiwa na majeraha mabaya sana. Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali za eneo hilo kwa ajili ya matibabu.

Jeshi lilisema limefanikiwa “kukabiliana na vikosi vya RSF” katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa mji.

Kulingana na taarifa yao, vikosi vya serikali vimewaua wapiganaji 80 wa RSF, na kuharibu magari yao 10, pamoja na kuwasababishia hasara kubwa.

RSF bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu matukio hayo ya jeshi.

Kumekuwa na makabiliano makali katika mji wa El-Fasher kati ya jeshi la Sudan na RSF tangu Mei 2024, licha ya jumuiya ya kimataifa kuonya kuwa mapigano katika mji huo ni hatari zaidi, kwa kuwa ni kitovu cha shughuli za misaada kwa majimbo yote matano ya Darfur.

Mapema wiki hii, RSF ilidai kuchukua udhibiti wa kambi ya wakimbizi ya Zamzam huko El-Fasher baada ya makabiliano na vikosi vya serikali. Raia wasiopungua 400 waliuawa na karibu watu 400,000 kuondoka eneo hilo kutokana na mapigano, hii ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Tangu 15 Aprili, 2023, wapiganaji wa RSF wamekuwa wakikabiliana na jeshi la serikali kwa lengo la kuchukua udhibiti wa nchi, jambo lililosababisha maelfu ya watu kuuawa na kuwa na moja ya hali mbaya kwa raia kote duniani.

Zaidi ya watu 20,000 wameuawa kufikia sasa na milioni 15 kuondolewa katika makazi yao, hii ni kulingana na Umoja wa Mataifa na serikali za mitaa. Hata hivyo, utafiti kutoka kwa wanazuoni wa Marekani, unakadiria idadi ya waliouawa kuwa karibu 130,000.

Katika wiki za hivi karibuni, RSF imepoteza maeneo mengi kote nchini Sudan baada ya jeshi kuwakabili.

CHANZO:АА
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us