Nchi 12 za kimataifa kupitia taarifa ya pamoja ya balozi zao zimeiomba serikali ya Kenya kuhakikisha usalama kwa waandamanaji huku vijana wakitangaza nia ya kuingia barabarani 25 Juni.
“25 Juni ni mwaka mmoja tangu Wakenya walipojitokeza kuelezea mahitaji yao kupitia maandamano yaliyoenea katika Mswada wa Fedha wa 2024,” taarifa ya balozi hizo zilisema.
“Wakati wananchi wakijiandaa kuadhimisha kumbukumbu hii tunatoa wito kwa wote kuwezesha maandamano ya amani na kujiepusha na vurugu.”
Balozi hizo pia zimeonya kuhusu wale wanaowashambulia waandamanaji.
“Tuna wasiwasi ya watu wasio na nia njema wanaojipenyeza au kuvuruga mikusanyiko ya watu wakati wa maandamano.”
“Matumizi ya polisi wa kawaida kwenye gari zisizo na kitambulisho yaliondoa imani ya umma na kuamuliwa kuwa ni kinyume cha sheria na mahakama kuu, tunaomba hili lifuatwe,” taarifa yao imesema.