Kuporomoka kwa shimo kumesababisha vifo vya takriban watu 16 katika mgodi mkubwa wa madini ya coltan katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, unaodhibitiwa na wanamgambo wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, duru za ndani ziliiambia Shirika la Habari la AFP siku ya Ijumaa.
Tangu kuzuka kwa vita tena mwaka wa 2021, M23 imechukua sehemu kubwa ya eneo la mashariki yenye rasilimali nyingi za DRC, na kuuteka mgodi wa Rubaya katika jimbo la Kivu Kaskazini mwezi Aprili 2024 kwa kusaidiwa na Rwanda.
Kuendelea kwa kundi hilo kudhibiti maeneno mapya kumezidisha mzozo uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu ambao umekumba eneo la mashariki mwa DRC, ambapo makumi ya makundi hasimu yenye silaha na mataifa ya kigeni yamekuwa yakigombea kwa muda mrefu udhibiti wa madini ya thamani katika eneo hilo.
Mgodi wa Rubaya unazalisha asilimia 15 hadi 30 ya madini ya coltan duniani ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki zikiwemo ‘laptop’ na simu za mkononi.
Wachimbaji walioathirika
Wakati wa maporomoko ya ardhi siku ya Alhamisi asubuhi, karibu wachimbaji 131 walikuwa kwenye eneo hilo, kulingana na Emmanuel Ndizeye, afisa wa eneo hilo aliyeteuliwa na kundi la M23.
Kati ya hao, 111 waliokolewa, huku miili 16 ikitolewa na wengine wanne bado hawajulikani walipo, msimamizi wa M23 eneo la Masisi ambako mgodi huo upo aliiambia AFP.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, M23 imeunda utawala sambamba na nchi ya Congo ili kudhibiti uendeshaji wa mgodi wa Rubaya tangu kudhibitiwa kwake.
Wataalamu hao wanakadiria kuwa M23 inapata takriban dola 800,000 za Marekani kwa mwezi kutokana na mgodi huo ikiwemo ushuru wa dola saba kwa kilo kwa uzalishaji na uuzaji wa coltan.
Mapato ya M23
Hata hivyo, kiasi hicho kinawakilisha sehemu ndogo tu ya mapato ya M23 kutokana na kodi zinazotozwa kupitia biashara katika mikoa iliyo chini ya udhibiti wake.
Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa pia wanaishutumu Rwanda, ambayo inakanusha kuwapa M23 msaada wa kijeshi, kwa kutumia wanamgambo hao kunyakua utajiri wa madini wa DRC.
Kando na kuwa na kati ya asilimia 60 hadi 80 ya coltan duniani, eneo la mashariki mwa DRC pia lina hifadhi kubwa ya dhahabu na bati.
Makampuni kadhaa ya kimataifa ya uchimbaji madini yamesitisha kwa muda shughuli zao mashariki mwa nchi kutokana na udhibiti wa meaneo unaoendelea wa kundi la M23.