AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania yatishia kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa za Malawi
Waziri Bashe amewashauri wasafirishaji wote wa Kitanzania kuacha kupakia bidha hizo mpaka mgogoro huo wa kibiashara utakapopata utatuzi.
Tanzania yatishia kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa za Malawi
Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo Tanzania. Picha-FB@Hussein Mohammed Bashe / Others
17 Aprili 2025

Serikali ya Tanzania imesema imepokea taarifa rasmi ya serikali ya Malawi ya kuzuia kuingia nchini humo kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashe, baadhi ya mazao hayo, ni pamoja na unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi.

Waziri Bashe amesema hatua hiyo ya Serikali ya Malawi imeathiri shughuli za wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kwenda nchini Malawi.

Kufuatia hatua hiyo, na kukiri kwamba kumekuwepo na juhudi za kidiplomasia kati ya nchi hizo ambazo hazijafanikiwa, Waziri Bashe ametoa maagizo yafuatao:

"Iwapo Serikali ya Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano ijayo, serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili," ameandika Waziri Bashe na kuongeza, "Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyengine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa."

Waziri Bashe amewashauri wasafirishaji wote wa Kitanzania kuacha kupakia bidha hizo mpaka mgogoro huo wa kibiashara utakapopata utatuzi.

"Usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania," amesema.

Wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara, wanasema kwamba, mgogoro huu wa kibiashara kati ya nchi hizo jirani, unaweza kuwa na athari kubwa zaidi hasa kwa Malawi ambayo haina bahari, na kwa kiwango kikubwa inategemea bidhaa za Tanzania na bandari ya Dar es Salaam katika uingizaji na utoaji wa bidhaa zake.

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa nchi hizo mbili kuingia katika mgogoro. Itakumbukwa kwamba, mwaka 2024, Malawi ilipiga marufuku mahindi ya Tanzania kuingizwa nchini mwake kwa madai ya mahindi hayo kuwa na sumu. Hata hivyo, marufuku hiyo baadae iliondolewa.

Lakini mwaka 2012, Tanzania na Malawi ziliingia katika mgogoro mkubwa zaidi wa kidiplomasia kufuatia mpaka wa Ziwa Nyasa/Malawi.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us