Chama cha Democratic Alliance nchini Afrika Kusini kimefungua kesi ya rufaa ya kutaka kuzuiwa kwa ongezeko la asilimia moja ya Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT kwa kipindi cha miaka miwili ya mwaka wa fedha ambayo iliainishwa katika bajeti iliyopitishwa Jumatano kwa kura nane.
Viongozi wakuu wa DA pia watakutana Alhamisi kuzingatia nafasi yake katika umoja wa vyama 10, mwenyekiti wa baraza la shirikisho Helen Zille amewaambia waandishi wa habari.
"Tunajua kwamba kuwa katika muungano kunahitaji kukubali baadhi ya mambo," amesema. "Huwezi kupata kila kitu. Lakini ANC pia haiwezi kupata kila kitu, na wanakataa wazi, kugawana madaraka."
Chama cha DA kiliungana na ANC katika serikali ya umoja iliyoundwa Juni 2024 baada ya ANC kushindwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi.
Matokeo yake, kinashika nafasi sita muhimu katika baraza la mawaziri.
"Tunajua uamuzi wowote tutakaouchukua utakuwa na athari kubwa kwa Afrika Kusini na uchumi. Kwa hiyo hatuna haraka ya kufanya uamuzi wowote," amesema Zille.
Chama hicho mara kadhaa kimekuwa na kikitofautiana na ANC ndani ya serikali ya umoja, ikiwemo kuhusu sera ya elimu na mipango ya bima ya afya ya taifa.
Viongozi waandamizi wa ANC pia wametilia shaka mustakbali wa muungano baada ya DA kuikataa bajeti, na kusema kwamba chama hakiwezi kuwa sehemu ya serikali iwapo kinakataa bajeti yake.
Serikali ya umoja imesifika kwa kuleta utulivu katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Afrika.
Vyama vyengine vikuu vya upinzani ni kile cha Wapigania Uhuru wa Uchumi na MK ambavyo pia vimeikataa bajeti ya Jumatano, na kusema kwamba serikali inahitaji kutafuta vyanzo vyengine kukuza uchumi kuliko kuwatoza kodi wananchi wa kawaida.
br/jcb/kjm