Maelfu ya mashabiki wa mashindano ya kitaifa ya utamaduni na filamu wamemiminika katika mji wa Nakuru nchini Kenya katika mashindano ya 63 yanayojumuisha wanafunzi wa ngazi zote nchini humo.
Kuanzia shule za chekechea hadi vyuo vikuu, maelfu ya wanafunzi watapata fursa ya kuonyesha talanta zao katika nyanja mbali mbali ikiwemo ngoma za kitamaduni, uigizaji wa majukwaani na wa filamu, mashairi, upigaji ngoma na mengineyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘ Utumiaji Teknolojia Kukuza Vipaji’
Matamasha haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka ambapo yamesaidia kukuza vipaji na hata kusaidia kuongoza vijana katika taaluma zao katika maisha.
Msingi wa vipaji
Na naam, wengi wa wasanii maarufu nchini Kenya wakiwemo waigizaji na watangazaji maarufu watanakiri kuwa chimbuko la vipaji vyao vimetokana na matamasha hayo.
“Kwa wanafunzi, ni uwanja wa kuonyesha utamaduni wao wa asili na kujifunza kutoka kwa wengine,’’ anasema Fredrick Masambaya, mmoja wa wakufunzi wa densi za kitamaduni katika tamasha hizo. ‘‘Muhimu zaidi ni kuwa matamasha hayo yanasaidia kufungua macho ya washiriki kutambua sanaa na maigizo yanavyoweza kuwa kazi endelevu kwao katika siku zijazo,’’ anaongeza.
Matamasha haya yamepanuliwa kila mwaka kujumuisha fani mpya, kuendana na ukuaji wa kijamii na teknolijia.
Mbali na densi za kitamaduni na uigizaji wa jukwaani na filamu, mwaka huu unaweza kupata pia usomaji wa podcast na hata usomaji habari kama fani zinazoshindaniwa.
Ubunifu kama kitega uchumi
Wizara ya Elimu, inayoandaa Tamasha hilo imesisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa washiriki katika kukuza utangamano wa watu wa matabaka yote.
‘‘Tamasha hili limekua tukio la kitaifa lenye upana na linalojumuisha wote. Linaangazia fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na podcast, uigizaji wa filamu na utangazaji wa moja kwa moja unaoangazia mageuzi makubwa ya kujieleza kwa ubunifu,’’ amesema Profesa Julius Bitok, Katibu katika Wizara ya Elimu.
Katibu Bitok pia alihimiza umuhimu wa kukuza vipaji kwa ajili ya kujipatia ajira ndani ya uchumi unaokua kwa kasi wa fani ya ubunifu.
‘‘Mtaala mpya uliotolewa wa elimu unawezesha wanafunzi kukuza vipaji vyao na kuchagua kufuatilia usanii kama somo lao kuu, kwa hivyo wataweza kugeuza kuwa kitega uchumi,’’ alisema Balozi Bitok.
Zawadi nono
Tamasha hili litaendelea hadi Aprili 14, ambapo washindi wa kitaifa katika fani zote watatangazwa na kupata fursa kuonyesha vipaji vyao mbele ya Rais katika hafla kuu ya kufunga.
Washindi pia watapewa vyeti na vikombe, pamoja na kitita cha fedha kinachotolewa na wadhamini wa tamasha.