Michael Olunga: Injinia wa kucheka na nyavu kutoka Kenya
Michael Olunga: Injinia wa kucheka na nyavu kutoka Kenya
Olunga almaarufu, ‘Injinia’ kutokana na taaluma yake ya uhandisi, ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya na mshambuliaji wa klabu ya Al Duhail ya nchini Qatar.
17 Aprili 2025

Michael Olunga Ogada mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akiichezea timu ya Al Duhail tangu mwaka 2021 na kuanzia wakati huo amekuwa moto wa kuotea mbali.

Olunga almaarufu, ‘Injinia’ kutokana na taaluma yake ya uhandisi, ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya na mshambuliaji wa klabu ya Al Duhail ya nchini Qatar.

Kwa sasa, yeye ndiye mwenye kuongoza kwa magoli mengi kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Abdullah bin Khalifa, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 10,000, ambao uko jijini Doha.

Darasani hadi uwanjani

Safari ya Olunga ya soka ilianzia akiwa shule ya sekondari ya Upper Hill iliyopo jijini Nairobi na baadaye akapata fursa ya kwenda kufanya majaribio nchini Ufaransa.

Hata hivyo, nyota ya Olunga ilianza kung’aa wakati akiicheza kwenye Ligi Kuu ya Kenya.

Kutoka Tusker hadi K’Ogalo

Aliichezea timu za Tusker na Thika United kabla ya kujiunga na mabingwa wenye historia katika ligi ya Kenya msimu wa 2015, Gor Mahia.

Alimaliza msimu huo akiwa mfungaji bora, akiwa ametupia wavuni mabao 19, na kuisaidia K’Ogalo wakati huo kushinda taji lake la 15, ikiwa hawajapoteza hata mchezo mmoja.

Mwaka 2016 na 2017,  ‘Injinia Olunga’ alicheza nchini Sweden na pia nchi China akiwa na klabu ya Guizhou Zhicheng.

Ligi ya La Liga

Mwaka 2017 alijiunga na timu ya Ligi ya nchini Hispania, Girona FC kwa mkopo wa mwaka mmoja huku msimu wa mwaka 2018, akicheza mechi yake ya kwanza, ambapo walipata ushindi wa magoli 6-0 dhidi ya La Palmas.

Olunga alifunga ‘hat-trick’ ndani ya dakika 22 tu.

Kwa mafanikio haya alikuwa Mkenya wa kwanza na mchezaji wa kwanza wa Girona kufunga hat-trick katika mechi ya ligi kuu ya Hispania.

Aliendeleza uhodari huu wa ushambuliaji akiwa na timu ya Kashiwa Reysol ya Japan 2018 na akawa mfungaji bora 2020 akiwa na magoli 28.

Al-Duhail ya Qatar

Ilipofika mwaka 2021, Olunga alitia nanga Al-Duhail kwenye ligi kuu ya Qatar Stars League na mwaka huo huo akafunga na ‘hat-trick’.

Misimu miwili iliyofuata akawa mfungaji bora wa ligi na pia kusaidia timu yake hiyo kushinda ligi msimu wa 2022-2023.

Kwa sasa yeye ndiye mfungaji mwenye magoli mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo ambayo uwanja wake wa nyumbani ni dimba la Abdullah bin Khalifa lililoko mjini Doha na lenye uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya 10,000.

Timu ya Taifa

Huenda akawa mfungaji mwenye magoli mengi zaidi kwa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars. Katika mechi zaidi ya 60 alizocheza amefanikiwa kucheka na nyavu mara 32.

Anayeshikilia rekodi hiyo kwa sasa ni William ‘Chege’ Ouma mwenye jumla ya magoli 35.

Ouma aliichezea Harambee Stars mara 66 kati ya 1965 na 1977. Anayemfuata Ouma kwa magoli mengi ya timu ya taifa ni Dennis ‘The Menace’ Oliech mwenye jumla ya magoli 34 na aliichezea Kenya mara 76 na alikuwa mshambuliaji wa timu hiyo kati ya 2002-2015.

Katika mechi ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi Machi ambapo Kenya ilifungwa magoli 2-1 na Gabon mjini Nairobi, Olunga ndiye aliyeweka kambani bao la kufutia machozi mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Baadaye aliwashukuru mashabiki kwa ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa X, akisema:

"Asanteni sana Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi kushabikia Harambee Stars. Licha ya kupoteza (2-1), wachezaji walijitahidi kadri ya uwezo wao. Napenda kutoa shukrani zaidi kwa wote waliofanikisha jambo hili. Asanteni sana mashabiki. One Love KENYA," Olunga aliandika kwenye ukurasa wake X.

Na huyo ndiye Olunga na mpira, Injinia anayeendeleza ufundi uwanjani.

 

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us