Kitivo cha Sayansi ya Afya cha Recep Tayyip Erdoğan cha Mogadishu, Chuo kishiriki cha Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya (UHS), kimekuwa na hafla ya kufuzu kwa wahitimu 172 iliyofanyika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Ikiwa sehemu ya mpango wa kuwa na wataalamu wa afya, hafla hiyo ya Jumatatu ilikuwa na furaha, bashasha, na tafakari kwa watu, kusisitiza msimamo wa taasisi hiyo wa ‘’ubinadamu kwanza’’.
Ikiongozwa na Amidi Profesa Dkt. Raşit Gündoğdu, hafla hiyo iliwaleta pamoja maafisa wa serikali ya Somalia, Balozi wa Uturuki mjini Mogadishu Alper Aktaş, wawakilishi kutoka taasisi za Uturuki waliyoko Somalia, na familia za waliohitimu.
Profesa Dkt. Kemalettin Aydın wa UHS alishiriki kwa njia ya mtandao. Katika hotuba yake muhimu, alisisitiza kuwa hafla hiyo ilikuwa zaidi ya kufuzu.
“Hafla hii ya leo siyo tu kuhusu kuwapa wanafunzi shahada. Inaashiria kuungana kwa pamoja kwa misingi ya undugu na kwa mioyo ya kusadiana. Katika maeneo ambayo yametelekezwa na mifumo ya dunia na kufilisiwa kutokana na mifumo ya ukandamizaji, ni fahari yetu kuandaa wataalamu wa afya wenye mafunzo, huruma, na mapenzi kwa ubinadamu,’’ Aydın aliongeza.
‘Mtazamo wa matumaini’
‘’Kama UHS, tunafanya zaidi ya kutoa mafunzo — tunaleta umoja na kutimiza jukumu letu la kihistoria. Kila mhudumu wa afya aliyepewa mafunzo Somalia pia atakuwa ni sauti ya wale waliokandamizwa na matumaini kwa ubinadamu,’’ alisema.
‘’Katika hafla hii, ningependa kumuenzi Sultan Abdulhamid II, ambaye aliweka msingi wa elimu kwa chuo kikuu chetu karne nyingi zilizopita kwa kuanzisha Mekteb-i Tıbbiye-i Şahane, kuweka pamoja elimu na huruma kwa watu akiwa na mtazamo wa kutoa msaada,’’ alisisitiza.
‘’Pia natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais Recep Tayyip Erdoğan, ambaye alifufua dira hii katika enzi hizi za kisasa kwa kuanzisha chuo chetu 2015 na kuongoza katika elimu ya afya duniani’’
Alisema chuo hicho kitaendelea kutoa ‘’mtazamo wa matumaini siyo tu nchini Uturuki lakini katika kila sehemu kwa kuimarisha utamaduni wetu na wengine’’ na hiyo ni ‘’huduma kwa Mungu na ubinadamu.”
Balozi wa Uturuki nchini Somalia Alper Aktaş alieleza kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Somalia umeimarika zaidi ya urafiki na kuwa ushirikiano wa kimkakati.
Alisema kuwa Chuo cha Sayansi ya Afya cha Recep Tayyip Erdoğan mjini Mogadishu kimekuwa mfano mzuri wa mafunzo ya afya siyo tu Somalia bali kote barani Afrika.
‘Tunafanya kazi kwa bidii ili tufanikiwe’
Alithibitisha dhamira ya Uturuki kuendelea kuunga mkono Somalia katika maeneo ya afya, elimu, na misaada kwa watu.
Waziri wa Elimu wa Somalia Nura Mustaf Mukhtar aliangazia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hasa enzi ambazo Uturuki iliposaidia watu wa Somalia 2011.
“Leo, tunashuhudia namna gani hizi mbegu zilivokuzwa na kuwa mti thabiti,” alisema. Waziri Mukhtar akieleza fahari yake kwa waliohitimu—hasa wale kutoka idara za Msaada wa Dharura na Usimamizi wa Majanga —na kuwapongeza wote, akitaja hasa miradi ya Uuguzi na Ukunga.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Fowsiya Abdikadir alisema kuwa elimu ya UHS imewapa siyo tu mafunzo ya kitaaluma lakini pia imewapa uwezo wa kukabiliana na majukumu.
“Tumefanya kazi kwa bidii kufika hapa. Nashkuru sana kwa chuo kikuu chetu na wote wale waliotuunga mkono katika safari hii ,” alisema.
Hafla hiyo ilikamilika kwa wahitimu kupewa shahada zao, sherehe ya kurusha kofia juu, na kupiga picha ya pamoja.