AFRIKA
2 dk kusoma
Sudan Kusini yaadhimisha siku ya uhuru
Sudan Kusini ilipata uhuru Julai 9, 2011
Sudan Kusini yaadhimisha siku ya uhuru
Sudan Kusini ilipata uhuru 9 Julai 2011/ picha: Reuters
9 Julai 2025

Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwaka 2011 baada ya kura ya maoni ambapo watu wake walipiga kura kwa wingi kujitenga na Sudan.

Uhuru ulikuwa kilele cha mapambano ya muda mrefu ya silaha yaliyoendeshwa na Wasudan Kusini kuanzia katikati ya miaka ya 1950.

Julai 9, 2011 Rais Salva Kiir aliongoza nchi hiyo kwa uhuru.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye mvutano wa kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar ulizua vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Zaidi ya watu milioni 2.2 walikimbilia nchi jirani na wengine zaidi ya milioni 2.2 wakahama makazi yao ndani ya nchi.

Makubaliano ya amani ya 2018 bado hayajaleta amani, ikiwa sasa rais Salva Kiir amemuwekea chini ya kifungo cha nyumbani makamu wake Riek Machar, tangu mwezi Machi 2025.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf ametoa pongezi zake kwa serikali na watu wa Sudan Kusini kwa kuadhimisha Siku hiyo ya uhuru wao.

“Siku hii inaashiria hatua muhimu katika safari ya Sudan Kusini kuelekea uhuru, umoja na ujenzi wa taifa,” amesema katika taarifa.

Amesema Umoja wa Afrika unapongeza uthabiti na azma ya watu wa Sudan Kusini na kusimama katika mshikamano na matarajio yao ya amani, utulivu na maendeleo.

“Umoja wa Afrika unasalia na nia thabiti ya kufanya kazi bega kwa bega na Sudan Kusini ili kuendeleza ushirikiano wa kikanda, kukuza maendeleo endelevu, na kudumisha maadili ya pamoja ya Pan-Africanism na umoja,” Youssouf ameongezea.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us