Rais William Ruto wa Kenya amewaelekeza maofisa wa polisi nchini humo kuwapiga risasi za miguuni watu watakaopatikana wakipora maeneo ya biashara na kuharibu mali wakati wa maandamano.
"Yeyote anayechoma biashara na mali za mtu mwingine, basi apigwe risasi mguuni na aende hospitalini kabla ya kupelekwa mahakamani. Ndio, msiwaue, ili muwapige risasi za miguu. Kuharibu mali za watu si sawa," alisema.
Kiongozi huyo ameyasema hayo wakati akizindua mradi wa kujenga nyumba 540 za makazi ya polisi katika eneo la Kilimani jijini Nairobi, Julai 9, 2025.
“ Wanaoshambulia Wakenya, maafisa wa polisi, mitambo ya usalama na biashara ni magaidi. Vitendo hivyo vya uhalifu ni tangazo la vita. Hatutakubali nchi yetu iharibiwe na wanaotafuta njia za mkato za kuingia madarakani,” alisema Rais Ruto.
Kauli ya rais inakuja huku kukiwa maandamano mwezi Juni na Julai ambapo mali ziliharibiwa na kuibiwa katika sehemu tofauti za nchi hiyo.
Vile vile, kiongozi huyo aliwaonya viongozi wa kisiasa ambao hawakutajwa majina yao kwa kuwachochea vijana kufanya vurugu.
"Ni viongozi wanaofadhili vijana kutekeleza vitendo hivyo, na sisi tunawafuata!"
Alisisitiza kuwa kuwa mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi na vituo vyao vya kazi, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya Juni 25, yatachukuliwa kama ugaidi.
"Wale wanaoshambulia polisi wetu, vituo vya usalama, vikiwemo vituo vya polisi, wanatangaza vita. Ni ugaidi, na tutakabiliana nanyi kwa ufanisi mkubwa. Hatuwezi kuwa na taifa linaloongozwa na ugaidi na kutawaliwa na ghasia; haitafanyika chini ya utawala wangu," alisema Ruto.
Kwa upande wao, wakosoaji wameendelea kulaani ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha wakati wa maandamano yanayoongozwa na vijana.
Wakati huo huo, kumekuwa na wasiwasi juu ya kutumwa kwa wahalifu - vikundi vya vijana vilivyo na marungu na mijeledi kushambulia waandamanaji na kupora biashara.
Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya, jumla ya watu 31 wameuwawa na wengine 107 kujeruhiwa wakati wa maandamano ya Julai 7, 2025.
Pia, kulikuwa na matokeo ya uharibifu wa majengo ya biashara katika kaunti 15 nchini humo.
Polisi walioneshewa kidole cha lawama kufuatia mauaji ya watu 16, yaliyoripotiwa wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.