Makanisa yasiyopungua mawili na nyumba 95 zimechomwa moto katika mkoa wa Cabo Delgado nchini Msumbiji katika mashambulio ya hivi karibuni ambayo polisi wanalaumu makundi ya kigaidi.
Orlando Modumane, msemaji wa polisi wa Msumbiji (PRM), ameliambia shirika la habari la Anadolu siku ya Jumatano kuwa washukiwa hao wa ugaidi walivamia maeneo ya Nkole na Ngura katika wilaya ya Ancuabe siku ya Jumapili lakini baadaye wakaondoka, alafu kurejea siku ya pili.
“Walivamia maeneo mawili mchana kabisa, wakiwa na bunduki na mapanga, na baadaye kuchoma makanisa mawili na nyumba 95, walikimbia wakiwa kwenye pikipiki 15 za wakazi wa maeneo hayo. Hakuna taarifa zozote za vifo, lakini wengi wao walilazimika kuondoka eneo hilo kwa ajili ya usalama wao,” Modumane amesema. Hakutaja kuhusu tukio lolote mahsusi.
Tangu 2017, eneo hilo lenye utajiri wa gesi limekuwa likikabiliwa na machafuko ya watu wenye silaha yaliyosababisha watu 10,000 kuhama makazi yao ikiwemo wanawake na watoto, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya watoto (UNICEF).
Mwaka 2024 pekee, watu wasiopungua 349 waliuawa katika mashambulio, kulingana na utafiti wa shirika la ACSS, taasisi ya kitaaluma iliyoko chini ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani.