Shaka Zulu: Shujaa aliyetengeneza himaya yenye nguvu na kisha kuuwawa na ndugu zake
Shaka Zulu: Shujaa aliyetengeneza himaya yenye nguvu na kisha kuuwawa na ndugu zake
Jina la Mfalme Shaka Zulu linazidi kuvuma, takribani karne mbili baadaye, akiwa amejizoelea umaarufu kwa kutengeneza himaya yenye nguvu zaidi kupata kutokea Afrika.
31 Machi 2025

Kama kuna jina ambalo litazidi kukumbukwa barani Afrika, basi ni jina la Shaka Zulu.

Taifa hilo la karne ya 19 lilianzishwa kutoka safu ya milima ya Drakensberg, kuelekea kwenye fukwe za bahari ya Hindi.

Kabla ya kuanzisha himaya ya Zulu, Shaka alitwaa makabila kadhaa na kufanikiwa kuongoza himaya hiyo kutoka mwaka 1816 hadi 1828, kabla ya kuuwawa na ndugu zake.

Hata baada ya karne kadhaa, urithi na umaarufu wa Shaka Zulu bado unaishi.

Kuzaliwa kwa shujaa

Izibongo Shaka kaSenzangakhona alizaliwa mwanzo wa karne ya 19 na familia ya kichifu katika eneo ambalo lilikuja kujulikana kama KwaZulu-Natal, nchini Afrika Kusini.

Mama yake aliitwa Nandi, binti wa mfalme aliyekuwa ametengwa.

Kwa kuwa alikuwa amezaliwa nje ya ndoa, Shaka alituhumiwa kuvunja tamaduni za Kizulu, hali iliyomfanya anyayapaliwe akiwa bado mtoto mdogo.

Hali hiyo ilimpa ujasiri Shaka wakati anakuwa. Ari yake ya upambanaji ilikuja kugundulika na Dingiswayo, chifu mwenye nguvu ambaye aliamua kuendeleza kipaji chake.

Dingiswayo alimuingiza Shaka jeshini na kumfanya awe mpiganaji hodari vitani.

Ujenzi wa himaya

Kifo cha baba yake Shaka, aliyekuwa anaitwa Senzangakhona, kilibadilisha muelekeo wa maisha ya Shaka.

Taratibu, Shaka akaanza kudhibiti baadhi ya koo na makabila.

Pia alifanikiwa kutengeneza jeshi lenye nguvu wakati wake.

Historia itamkumbuka kwa mbinu zake za kijeshi zilizotilia mkazo kwenye shabaha.

Mbinu hizo zikawa maarufu katika mapambano dhidi ya ukoloni katika eneo la Kusini wa Afrika.

Ngome shupavu

Ilipofika miaka ya 1820, Mfalme Shaka alikuwa amegeuza himaya yake kuwa eneo lenye nguvu kutokana na mbinu zake za kijeshi, jambo lililoiwezesha kutwaa udhibiti wa maeneo mengine.

Shaka Zulu atakumbukwa kwa kuboresha matengenezo ya pinde ndefu, zilizojulikana kama “assegais” na “iklwas”.

Kuanguka kwa himaya

Hata hivyo, himaya yake haikuweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kipindi kile.

Anguko lake lilitokana na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya washirika na washauri wake.

Huzuni kubwa ilighubika maisha ya Shaka kufuatia kifo cha mama yake kilichotokea mwezi Septemba 1827, na ikamlazimu kutangaza mwaka mmoja wa maombolezo.

Uamuzi huo ulisitisha uvunwaji wa mazao na kusababisha njaa kali na mateso makubwa kwa watu wake.

Wale waliokaidi amri hiyo, waliuwawa na wengine kufukuzwa kutoka kwenye himaya hiyo.

Shaka alitengeneza mpasuko mkubwa kati yake na wale aliowatala.

Mwaka mmoja baada ya kifo cha mama yake, Shaka aliuwawa na ndugu zake Dingane na Mhlangana.

Na huo ndio ukawa mwisho wa utawala wa Shaka Zulu, shujaa wa kivita barani Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us