Kila Jumapili, Khadija Musa Sele na binti zake watatu huenda kwenye kibanda cha msusi aliye mtaani kwao jijini Nairobi, kwa lengo la kuonekana nadhifu.
Utamaduni huu wa miaka mingi hulenga kuwaandaa watoto kwa ajili ya mwanzo mpya wa juma.
“Hawa wawili wadogo nawasuka milazo, kwa sababu mtindo huo ni rahisi kuutunza na inachukua muda mfupi kusuka na kufumua, japo huyu mkubwa anapendelea zaidi mtindo wa Kilimanjaro, unaonakshiwa na mkia wenye kuning’inia,’’ anasema Khadija katika mahojiano yake na TRT Afrika.
“Lakini mimi mbinafsi napendelea milazo miwili tu au fundo moja.’’
Si ajabu kukutana na mitindo mbalimbali ya misuko katika pitapita zako maeneo mbalimbali barani Afrika.
Kimsingi, siku hizi misuko yote ni kutokana na mitindo na mapambo, au wakati mwingine urahisi tu wa kushika nywele.
Ishara ya kupinga utumwa
Hata hivyo, haikuwa hivyo nyakati za kale.
Kulingana na wabobezi wa historia za utumwa, ususi wa mtindo wa ‘conrows’ miongoni mwa watumwa, ulitumika wakati wa vuguvugu la mageuzi na ukombozi.
Kulingana na wanahistoria, wakati mwingine, mistari ya misuko kichwani, iliashiria njia za siri za kukwepa mashamba ya wakoloni na wazungu waliomiliki watumwa.
Wakati mwingine, ziliashiria mipango ya kukutana kwa siri na maeneo ya kukukutania pasipo kujulikana na wazungu. Mitindo hiyo, pia ilitumika kuficha Pia wangeficha vitu humo ndani ya mistari na kupitishiana bila wamiliki wao kujua.
Pia ilitumika kama ishara ya ukaidi kwani, miongoni mwa mambo mengine, wazungu waliwanyoa nywele watu wao kama namna ya kuwavua utambulisho na asili yao ya Kiafrika. Kimsingi, mitindo ya kusuka nywele iliwasaidia watumwa hao kukumbuka asili yao.
Mapambo kupitia usukaji
Hata hivyo, siku hizi mitindo ya kusuka nywele inawakilisha ulimbwende na sio ramani za kufikia ukombozi wala namna ya kujivunia asili ya mtu mweusi.
Ukifika pale kwa Msusi safi, utakutana na orodha ya majina ya mitindo mbalimbali ya usukaji nywele.
Kwa mfano, kuna ‘Kilimanjaro’, ambao ni mtindo unaoambaa kando kando ya kichwa na kukutana kwenye kisogoni. Pia upo wa milazo, ambayo ni mistari inayoteremka hadi mwishoni mwa kisogo na wakati mwingine kuwa katika hali ya kuning’inia.
Vile vile upo wa ‘Da Brat na ‘Twende Kilioni’ wa kisogo na wakati mwingine kuning’inia, ambazo zimejizoelea umaarufu Afrika Mashariki.
Ukisogea Afrika magharibi, utakutana na mitindo tofauti kama vile ‘Zane’ ambao unafanana na milazo ya Kiswahili, pia upo mtindo wa ‘Shuku’.
Katika kitabu chake kiitwacho Americanah, mwandishi maarufu wa riwaya na hadithi kutoka Nigeria, Chimamanda N’gozie anaandika “Nywele sio taarifa ya kisiasa-ni urithi, uzuri, fahari, sherehe ya Weusi.’’
Mila yenye kufifia
Hata hivyo kumekuwa madai kwamba utamaduni wa ususi wa nywele miongoni mwa Waafrika na Wamarekani, taratibu unafifia.
Kwa sasa, uchomaji wa nywele kwa njia ya moto na kemikali zingine unaendelea kushika kasi, jambo ambalo linaonekana hasa miongoni mwa jamii za waafrika wasomi, wanaopendelea zaidi kama taswira ya usomi.
Pia uvaaji wa nywele bandia unachukuliwa kama ishara ya kutoridhika na asili ya Uafrika, ya kuwa na nywele ngumu zilizosokotana.
“Mimi siwezi kuwapaka wanangu kemikali kichwani kwani ni hatari kiafya na inaweza kunyausha nywele zao,’’ Khadija anaiambia TRT Afrika.