UTURUKI
2 dk kusoma
Uturuki, Ufaransa zajadiliana uhusiano wa kikanda
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesisitiza haja ya kuongeza uratibu na nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya katika suala la usalama wa Ulaya.
Uturuki, Ufaransa zajadiliana uhusiano wa kikanda
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, siku ya Jumatano, wawili hao walitumia muda wao kujadili kwa kina masuala mbalimbali./Picha: AA
3 Aprili 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesisitiza haja ya kuongeza uratibu na nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya katika suala la usalama wa Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana na Jean-Noel Barrot,  waziri mwenzake kutoka Ufaransa, jijini Paris kujadiliana uhusiano wa mataifa hayo mawili na masuala mengine ya kikanda.

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, siku ya Jumatano, wawili hao walitumia muda wao kujadili kwa kina masuala mbalimbali.

Katika mazungumzo hayo, Fidan aliangazia suala la kuongeza uratibu na nchi zisizo wananchama wa Umoja wa Ulaya katika kuimarisha hali ya usalama barani Ulaya.

Pia, alionesha matarajio yake kwa Ufaransa, katika kuunga mkono kuondoa vikwazo vyenye kudumaza uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, na kwamba Umoja wa Ulaya utafuata muelekeo huo huo. Suala la uhuhishwaji wa Umoja wa Forodha kati ya Uturuki na Ulaya, ulijadiliwa wakati wa mazungumzo hayo.

Jitihada za kumaliza migogoro

Fidan alionesha utayari wa Uturuki katika kuunga mkono jitihada za kidiplomasia za kumaliza mgogoro kati ya Urusi na Ukraine na kutilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wanachama wote wa NATO wakati wa mchakato huo.

Kulingana na Fidan, kila suluhu lazima iwe na baraka kutoka pande zote mbili.

Kuhusu suala la Syria, Fidan alisisitizia umuhimu wa ushirikishwaji zaidi wa serikali mpya ya nchi hiyo huku akitaka nchi hiyo iondolewe vikwazo.

Fidan alionesha matarajio ya Uturuki hususani kwenye eneo la ushirikiano wa sekta ya viwanda vya ulinzi huku akisisitiza umuhimu wa kupambana na vikundi vya kigaidi vya PKK/YPG.

Pia, aliongeza kuwa magaidi wa Daesh waliowekwa mahabusu na kwenye kambi kaskazini mwa Syria, warudishwe makwao.

Ubabe wa Israeli huko Gaza

Kulingana na Fidan, mashambulizi ya Israeli yatasababisha kukosekana kwa utulivu wa kikanda huku akionesha msimamo wa Uturuki dhidi ya uhamishwaji wa lazima wa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao.

Hali kadhalika, aliunga mkono mpango wa Gaza, kama ulivyoasiliwa na jumuiya ya Kiarabu, akisisitiza kuwa hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya katika eneo hilo kutokana na Israeli.

Fidan alisisitiza umuhimu wa mchakato nyoofu wa kufikisha msaada huko Gaza.

Fidan na Barrot pia walijadiliana jitihada za amani na utulivu ndani ya Caucasus.

Wawili hao walipitia hatua za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuangazia fursa za ushirikiano katika sekta ya nishati.

Kulingana na Fidan, Uturuki inafuatilia kwa ukaribu yale yanayoendelea nchini Ufaransa.

CHANZO:TRT World and Agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us