AFRIKA
2 dk kusoma
Polisi wa DRC wavamia maeneo ya aliyekuwa Rais Kabila – familia
Wachunguzi wanasema walikuwa wanatafuta vifaa vya kijeshi ambavyo huenda "viliibiwa au vimefichwa" lakini hakuna kilichopatikana, hii ni kulingana na msemaji wa familia ya Joseph Kabila.
Polisi wa DRC wavamia maeneo ya aliyekuwa Rais Kabila – familia
Rais Felix Tshisekedi na Kabila waliunda muungano wa kugawana madaraka kufuatia uchaguzi ulioleta utata wa 2018. /Reuters
17 Aprili 2025

Maafisa wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamevamia maeneo yanayomilikiwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, ambaye alisema atarejea nchini kupitia upande wa mashariki, msemaji wa familia alisema Alhamisi.

Rais wa sasa Felix Tshisekedi amemshtumu Kabila kwa kupanga njama ya "uasi" na kuunga mkono muungano unaojumuisha kundi lenye silaha la M23 ambalo linapigana na serikali mashariki mwa DRC.

Maafisa wa usalama walimwambia meneja wa sehemu mojawapo, shamba la Kingakati, lililoko kilomita 80 mashariki mwa mji wa Kinshasa, kuwa "msako ulikuwa umepangwa," alisema Adam Shemisi, msemaji wa mke wa Kabila, Marie-Olive Lembe Kabila.

Maafisa wa usalama pia walivamia eneo lingine la familia ya Kabila lililoko Kinshasa, msemaji aliongeza.

Vifaa vya kijeshi

Kulingana na Shemisi, wachunguzi wanatafuta vifaa vya kijeshi ambavyo huenda "viliibiwa au vimefichwa" lakini hawakupata chochote.

Kabila alikuwa rais kwa miaka 18 hadi mwaka 2019 alipoondoka madarakani kutokana na maandamano.

Msemaji amesema Kabila, 53, aliondoka DRC kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2023.

Lakini wiki iliyopita, katika ujumbe uliosambazwa na wafanyakazi wake, alisema atarejea nchini kupitia mashariki kwa kuwa taifa liko katika "hali mbaya".

Hajasema tarehe


Bado hajasema ni lini atakaporejea, na haikufahamika kama atapitia katika maeneo ambayo kwa sasa yanadhibitiwa na kundi la M23.

Kundi hilo lenye silaha limeteka miji muhimu mashariki mwa DRC, ikiwemo Goma na Bukavu.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kimataifa wanasema kundi la M23 linaungwa mkono na Rwanda, madai ambayo Rwanda inakanusha.

CHANZO:AFP
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us