Watu wasiopungua 70 wameuawa na wengine kujeruhiwa baada ya wahalifu kuvamia walinzi wa sungusungu siku ya Jumatatu katika eneo la Kanam jimbo la Plateau, kaskazini kati mwa Nigeria.
Kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo, wengi wa waliouawa walikuwa sungusungu kutoka jamii mbalimbali walioitwa kuja kujadili mashambulizi katika eneo la Kanam.
Aliyu Baffa, mwenyekiti wa kundi hilo la sungusungu katika eneo lililovamiwa, alisema wahalifu hao waliwavamia sungusungu wakati wakielekea kujificha katika msitu unaojulikana maarufu kama Madam Forest.
“Tumewazika watu zaidi ya 60 na wasiopungua 70 wameuawa. Baadhi ya sungusungu waliokimbia wamethibitisha kuwa walizidiwa nguvu na wavamizi hao,” Baffa aliliambia shirika la Anadolu Jumanne.
Wengi wameachwa bila makazi
Wakazi, waliozungumza na Anadolu, wanasema wengi wameondolewa katika makazi yao kutokana na tukio hilo.
“Wavamizi hao wamewaua sungusungu ambao wanatulinda sisi, kwa hiyo ilikuwa lazima tuondoke katika eneo hili. Wamechoma nyumba zetu na kutufanya kukosa sehemu ya kuishi. Baadhi ya waliouawa walizikwa leo asubuhi,” anasema Kazeeem Muhammad, mkazi ambaye Jumatatu aliondoka jimbo la Plateau kwenda jimbo la Taraba.
Shapi’i Sambo, kiongozi wa vijana katika eneo lililoathirika, anasema juhudi zinaendelea kubaini idadi kamili ya wale waliouawa kwenye tukio hilo.
Polisi bado hawajatoa taarifa yoyote kuhusu mashambulizi hayo karibu saa 24 baada ya uvamizi huo. Alabo Alfred, msemaji wa Polisi Jimbo la Plateau, hakujibu alipotakiwa kufanya hivyo na Anadolu.
Changamoto za usalama
Uvamizi Nigeria, hasa katika kanda ya kaskazini magharibi na kaskazini kati, unachangia kuwepo kwa changamoto kubwa ya usalama. Makundi haya yanajulikana kwa ukatili wao, kuvamia vijiji, kuteka wanakijiji kwa lengo la kutaka kikombozi, na uporaji.
Ingawa Rais Bola Tinubu amechukuwa hatua kali dhidi ya wavamizi na magaidi nchini Nigeria, makundi hayo bado yanaendelea kutatiza amani nchini humo.