Sababu kuu ya maandamano nchini Kenya ilikuwa ni kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 ambao miongoni mwa masuala mengine ulipendekeza kupandisha kodi kwa baadhi ya bidhaa kuashiria kupanda kwa gharama za maisha.
Mwezi Mei vijana, bila kutumia jukwaa la kisiasa wakaanza kuhamasishana kupitia mitandao ya kijamii wakizungumzia vipengele muhimu vya mswada huo pamoja na kutafsiri kwa lugha kadhaa na lugha nyepesi inayofahamika na mwananchi wa kawaida.
Tarehe 18 Juni maandamano yakaanza mjini Nairobi na katika baadhi ya maeneo mengine, lakini bunge likapitisha mswaada huo.
Licha ya rais Ruto kusema kuwa hatotia saini mswada huo kutokana na kutoungwa kikamilifu na watu, maandamano yaliendelea na tarehe 25 Juni vijana wakavamia bunge, na wabunge wakatimka.
Watu wasiopungua 50 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Wengine walitekwa na kuteswa kwa kile ilichosemekana kuwa ni maafisa wa usalama.
Rais Ruto aliukataa rasmi mswada huo, lakini mwezi Julai Gen-Z wakaendeleza tena maandamano wakitaka ajiuzulu.
Kufikia Julai 11 Ruto akafuta baraza zima la mawaziri isipokuwa Naibu rais na waziri kiongozi, akiahidi kuunda serikali jumuishi.
Julai 17 polisi ikapiga marufuku maandamano jijini Nairobi, wakidai kuwa ni sababu za kiusalama. Siku iliyofuata mahakama ikabatilisha kauli hiyo ya polisi.
Julai 19 baadhi ya mawaziri wakarejeshwa kwenye baraza na wiki moja baadaye rais Ruto akatimiza ahadi yake ya serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwajumuisha wanasiasa wa upinzani kwenye baraza.
Huenda ikawa hali ilitulia kwa muda, lakini sauti za Gen-Z na wengine zimekuwa zikirindima kwa njia mbalimbali hasa katika mitandao ya kijamii kikubwa ikiwa ukakasi wa gharama za maisha.
Je, kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa kwa vijana hao, kutakuwa na tija yoyote?