Kenya: Maandamano ya Gen Z 'yaanika madudu' ya utendaji wa polisi
AFRIKA
4 dk kusoma
Kenya: Maandamano ya Gen Z 'yaanika madudu' ya utendaji wa polisiLicha ya malalamiko na madai ya ukatili wa polisi, Rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa serikali yake itaendelea kuiunga na Huduma ya Kitaifa ya Polisi, wanapoendelea kutekeleza majukumu yao.
Kenya police / Reuters
24 Juni 2025

Juni 25, 2025, wakenya wanaadhimisha mwaka mmoja toka yalipofanyika maandamamo ya Gen Z, tukio ambalo lilitikisa sio Kenya peke yake, bali la Afrika kwa ujumla.

Ujasiri wa vijana hao kupinga utawala wa Rais Ruto, hasa kutokana na mswada tata wa fedha wa mwaka jana, uliwaamsha wanaharakati mbalimbali, kuwashtua viongozi na hata kuviweka vyombo vya usalama tumbo joto.

Hali hiyo iliwalazimu kutumia mbinu za kila aina ili kuwadhibiti waandamanaji hao, na hivyo kufungua milango iliyopelekea kuchunguzwa undani.

Hanifa Safia ni mmoja wa waandamanaji walioonekana kuwakera na kuwaudhi polisi.

Kubebwa juu juu

“Nilipigwa na mmoja ya wahuni na kuchukuliwa simu yangu japo nilifanikiwa kuipata,” aliandika Hanifa kwenye ukurasa wake wa X, mara ya maandamano ya jijini Nairobi.

Picha mbalimbali za mjongeo, zimemuonesha Hanisa akibwebwa ‘mzobemzobe’ na kutupwa kwenye gari la polisi.

Madai haya, yalimlazimu Hanifa, kupitia chama cha wanasheria cha Kenya (LSK), kuwashitaki polisi mwezi Agosti mwaka jana, akiwatuhumu kutumia nguvu kupita kiasi wakati wakiwadhibiti waandamanaji hao.

Uamuzi wa mahakama

Kesi hiyo, iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, iliwalenga maofisa kadhaa wa polisi kwa utovu wa nidhamu wakati wa maandamano.

Kulingana na LSK, kutumwa kwa polisi waliovalia kiraia, kulifanikisha ukatili dhidi ya waandamanaji, kwani hawakuweza kutambulika kwa urahisi, na hivyo kuharibu pakubwa imani ya umma kwa mashirika ya kutekeleza sheria.

Jaji Bahati Mwamuye aliamuru maafisa waliovalia kiraia wasiruhusiwe kufunika nyuso zao wanaposhughulika na wananchi.

Polisi kujitambulisha

Kinyume chake, maafisa waliovaa sare watahitajika kuonesha vitambulisho vyao, majina yao na namba zao ili waweze kutambuliwa kirahisi. Hatua hii inakusudiwa kuongeza uwajibikaji na kutoa mfumo wa utambulisho kwa maafisa wakati wa mazungumzo ya umma.

Lakini tangu uamuzi huo wa mahakama, kumekuwepo na maandamano zaidi na bado polisi wanaendelea kutuhumiwa kwa uvunjaji na ukiukwaji wa kanuni nyingi za kudhibiti maandamano.

Inaripotiwa kuwa, kumekuwepo walau kifo kimoja katika kila maandamano, baada ya polisi kuwamiminia risasi waandamanaji, wengi wao wakiwa ni vijana.

DCI yatuhumiwa kwa ukatili

Baadhi ya vitengo vya ujasusi kama vile DCI, wameshutumiwa kuwateka washukiwa na waratibu wa maandamano hayo, wakiwazuia bila kuwafungulia mashitaka yoyote. Pia, wanadaiwa kuwatesa huku kukiwa na hofu kuwa huenda watu kadhaa wamefariki mikononi mwao wakati wa kuhojiwa.

Kwa mfano, wiki hii, ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Kenya, imeidhinisha kufunguliwa mashtaka kwa polisi watatu waliohusika na mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang’, aliyefia ndani ya kituo cha polisi.

Kifo cha Ojwang’ kiliibua ghadhabu na hasira ya umma, huku maandamano mapya yakiibuka.

Na, ni katika maandamano hayo, kamera zilimnasa polisi mmoja akimmiminia risasi kijana aliyekuwa akiuza barakoa barabarani. Tayari, polisi huyo ametiwa ndani baada ya ghadhabu ya umma.

Mbali na ukatili huo mikononi mwa polisi, vikosi vya usalama vimeshutumiwa kwa kughushi ripoti za vyumba vya kuhifadhia maiti, kutaja kuwa vifo vilisababishwa na risasi kuwa ajali au "kupigwa na umati ".

Msaada wa teknolojia

Lakini vijana waliojihami kwa simu za kisasa walidhihirisha matendo ya siri ya polisi hadharani.  Video zilizorekodiwa, zilionesha polisi wakitumia mabomu ya machozi, virungu, na hata kufyatua risasi za mpira dhidi ya waandamanaji.

Wakati wa maandamano ya Juni mwaka jana ya "kuvamia Bunge", IPOA ilirekodi vifo 39, majeruhi 150, na matukio 7 ya utekaji nyara.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya Human Rights Watch, ulibaini vifo vya waandamanaji 61 kutokana matukio ya kufyatuliwa risasi.

Kulingana na IPOA, kumekuwepo na ongezeko la malalamiko na ushahidi dhidi ya polisi ambapo kwa kiasi kikubwa, umeweka wazi ukosefu wa mafunzo ya kutosha au kuongezeka tabia ya uvunjifu wa sheria miongoni mwa watu waliokasimiwa majukumu ya kutekeleza sheria.

Lakini hali isiyo tarajiwa, Rais William Ruto wa Kenya, amesema kuwa serikali yake itaendelea kuiunga mkono Huduma ya Kitaifa ya Polisi wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Maandamano makubwa

Kulingana na Rais Ruto, polisi wana jukumu la kulinda taifa na kulinda maisha na mali za Wakenya.

‘Hakuna mhalifu atakayeruhusiwa kutumia nguvu dhidi ya polisi ili kuwadhoofisha na kuwatisha, akibainisha kuwa jambo hilo linadhoofisha usalama wa taifa,’’ aliongeza Rais Ruto. "Kwa kila afisa wa polisi, ninawapa hakikisho langu kwamba serikali ya Kenya itawaunga mkono, itasimama nanyi mnapolinda taifa letu na kuweka familia na mali zetu salama," akaongeza.

Sasa wengi wanauliza, tangazo la Rais kama alivyotoa wakati joto na hamaki dhidi ya polisi imepanda, itaongeza jeuri la polisi hao kuzidisha nguvu?

Hii inakuja baada ya msemaji wa serikali Isaac Mwaura kutangaza kuwa maandamano ya Jumatano hayajapewa idhini kufanyika. Gen Z wameyaita ‘mama ya maandamano yote’.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us