Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Ijumaa alishtumu vikali mashambulizi ya kijeshi ya Israeli huko Gaza, akiteta kuwa serikali ya Israeli inafanya ukatili dhidi ya Wapalestina, na kuzungumzia ukimya wa jumuiya ya kimataifa kuhusu suala hilo.
“Bila kujali wala kutofautisha, serikali ya Israeli inawaua kikatili watu wa Palestina,” Erdogan alisema wakati wa mkutano na wawakilishi wa mabunge yanayounga mkono Palestina mjini Istanbul, Uturuki, akizungumzia idadi kubwa ya vifo vya wanawake na watoto Gaza, pamoja na madaktari na wafanyakazi wa misaada wa kigeni na wa eneo hilo.
Akieleza kuwa wamekusanyika kupaza sauti kwa ajili ya Palestina, ambayo ni chimbuko la ustaarabu na sehemu ambayo kihistoria mitume wengi wametoka huko, Erdogan anasema kwamba leo wameungana siyo tu kutetea watu na ardhi yao, bali kutetea haki, amani, na ushujaa.
Akizungumza kuhusu matumaini yake kwamba mkutano huo na maamuzi yake yatafaidi Palestina, Erdogan aliwashkuru wabunge wote ambao wanalichukulia suala la Palestina kama la kwao na kuliunga mkono.
“Pamoja na haya yote, suala la Palestina, mapambano ya kuheshimu ubinadamu. Siyo tu suala la Waislamu ila ni suala la binadamu yoyote mwenye kuzingatia utu. Hakika, suala hili ni zaidi ya siasa – ni zaidi ya suala la utu,” alisema.
Kwa miezi kadhaa, “vyombo vya habari duniani na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa kimya wakiangalia jambo hili likifanyika” huku waandishi wa habari na watoto wakiuawa, aliongeza.
“Zaidi ya 7% ya watu wa Gaza wameuawa au wana majeraha ya muda mrefu. Zaidi ya waandishi wa habari 212, ambao walikuwa wanatoa taarifa za ukweli kutoka eneo hilo, wameuawa. Juzi juzi tu, mwandishi wa kike alikufa shahidi akiwa na watu 10 wa familia yake. Mamia ya madaktari, wauguzi, na wahudumu wa afya walifyatuliwa risasi. Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wameuawa. Watoto wachanga wanakufa tukiwaona kutokana na kukosa dawa, maji, na chakula.
“Tuna kundi la watu ambalo halina utu kabisa kiasi cha kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa watoto wao kwa kuuwa watoto wa Palestina. Shule, makanisa, miskiti, na vyuo vikuu vimeshambuliwa kwa mabomu. Majengo ya Gaza karibu 80% yameharibiwa. Gaza imeharibiwa kiasi kwamba hakuna hata jiwe moja limebaki. Kuna vifusi vya zaidi ya tani milioni 50,” aliongeza.
‘Undumakuwili’ wa mataifa ya Magharibi
Akishtumu mataifa ya Magharibi kwa kuwa na undumakuwili, Erdogan alisema: “Wakiona jambo kidogo tu kwingine, wanaweka vikwazo haraka. Lakini nauliza, mbona hawafanyi hivyo dhidi ya Israeli?”
Rais alisema karibu Wapalestina 60,000 “wameuawa kikatili” tangu Oktoba 7, 2023, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuonya kuwa “pendekezo lolote la kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao walioishi kwa maelfu ya miaka halina msingi.”
Erdogan alisisitiza kuwa suala la Palestina ni “mapambano ya kutafuta heshima” na msimamo wa kutetea “ubinadamu, amani, na haki,” akitoa wito kwa jamii ambayo imepitia “mauaji ya halaiki miaka 75 iliopita” ipaze sauti yake na kuwaambia viongozi wake “kusitisha mauaji,” bila shaka akizungumzia mauaji ya Kinazi dhidi ya Wayahudi.
Aliwashtumu wale wanaokaa kimya kuhusu mauaji ya Gaza kwa kujaribu “kushabikia mauaji ya halaiki” na kuyaita mapambano ya Wapalestina "ugaidi."
“Tangu Oktoba 7, 2023, kaka na dada zetu wa Gaza na Wapalestina wamepitia ukatili mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha karne moja iliyopita,” Erdogan aliongeza.