Usichokijua kuhusu mavazi maarufu yatokanayo na magome ya miti ya mikuyu nchini Uganda
Usichokijua kuhusu mavazi maarufu yatokanayo na magome ya miti ya mikuyu nchini Uganda
Katika mila ya Baganda nguo hizo huvaliwa wakati wa kutawazwa kwa wafalme, matambiko na matibabu ya kitamaduni na hata mazishini.
11 Aprili 2025

Katika jamii ya Baganda, mti wa Mkuyu ni kati ya miti yenye kuthaminiwa sana.

Kwa miaka mingi sasa, miti hiyo Mti huu, ambao kwa lugha ya eneo hilo hujulikana kama ‘Mutuba’, hutoa magome yenye kutengenezea mavazi kwa miaka mingi sasa.

Watu maalumu, waitwao “Ngonge”, ndio waliohusika na utengenezaji wa vitambaa kutoka magome hayo kwa ajili ya familia ya kifalme ya Baganda na jamii nzima kwa ujumla.

Mafundi hawa hurithisha ujuzi huu, toka kizazi kimoja hadi kingine.

Uvunaji magome

Mchakato huu hufanyika kwa ustadi mkubwa bila kuharibu miti.

Uvunaji wa magome haya hufanyika zaidi wakati wa misimu ya mvua.

Magome haya huchongwa na kuvunwa kutoka kwenye miti kabla ya kuwekwa kwenye maji ya moto ili kuua vijidudu na vimelea vingine.

Baada ya kuwekwa kwenye maji ya moto, magome hayo hugongwa na kitu kizito kama nyundo ili kuilainisha, kuinyoosha na kuikausha.

Miti ya mikuyu huvunwa kila mwaka kwa kipindi cha miaka 40, ikitoa hadi mita 200 za mraba kwa nguo moja moja.

Ili yasikauke kwa haraka, mafundi wa magome haya huyafanyia kazi ndai ya banda maalumu lililo wazi.

Mabadiliko

Kuanzia karne za 14, mavazi yatokanayo na magome yalivaliwa na familia ya kifalme pekee.

Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa sasa, kwani nguo zitokanazo na magome ya mikuyu huvaliwa na rika zote.

Licha ya kitambaa cha kawaida kutoka kwenye magome ya mikuyu kuwa na mseto wa rangi ya huzurungi na nyekundu, kitambaa cha gome cha wafalme na machifu hunakshiwa kwa rangi nyeupe  au nyeusi na huvaliwa kwa mtindo tofauti ili kusisitiza hadhi yao.

Mavazi maalumu

Katika mila ya Baganda nguo hizo huvaliwa wakati wa kutawazwa kwa wafalme, matambiko na matibabu ya kitamaduni na mazishini pia.

Majumbani, vitambaa vitokanavyo na miti ya mikuyu  hutumiwa kwa mapazia, vyandarua na hata matandiko maalumu.

Hata hivyo, huenda mavazi haya yakapoteza umuhimu wake, hususani kutokana na ujio wa mavazi ya kisasa, licha ya wataalamu wa mitindo mbalimbali kuendelea ‘kuumiza vichwa vyao’, ili kuhakikisha kuwa umuhimu wa mavazi haya unabaki pale pale.

Kwa mfano, wapo walioweza kubuni mitindo mipya kupitia kofia, mabegi na vitu vingine.

Hata hivyo, ni jambo la kutia moyo kuona, shirika la Umoja wa Mataifa, Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), likitambua ujuzi wa jamii ya Wabaganda, hasa katika utengenezaji wa nguo zitokanazo na magome ya mikuyu.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us