AFRIKA
2 dk kusoma
Lesotho yatangaza janga la kitaifa kutokana na ukosefu wa ajira
Lesotho imetangaza kuwepo kwa "janga la kitaifa" kutokana na kuongezeka kwa idadi ya ukosefu wa ajira na kuendelea kupotea kwa ajira zaidi kutokana na kudorora kwa uchumi na ushuru wa Marekani.
Lesotho yatangaza janga la kitaifa kutokana na ukosefu wa ajira
Waziri Mkuu wa Lesotho Sam Matekane anasema vijana wa nchi hiyo ‘’wanahitaji msaada’’ wa ajira. / TRT Afrika English
8 Julai 2025

Nchi ya Kusini mwa Afrika ya Lesotho imetangaza hali ya "janga la kitaifa" kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na kupotezwa kwa nafasi za kazi wakati nchi ikikabiliwa na mdororo wa uchumi kutokana na ushuru wa Marekani na kusitishwa kwa misaada.

Uchumi wake unategemea sekta ya kutengeneza nguo ulikuwa tayari unakabiliwa na idadi kubwa ya ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, kabla Rais Donald Trump kupunguza misaada na kuweka vikwazo vya biashara.

Sheria hiyo – ambayo inawapa serikali uwezo zaidi ikiwemo kwenda nje ya utaratibu uliowekwa – itatumika kwa miaka miwili, kulingana na tangazo rasmi la serikali la tarehe 7 Julai.

Tayari wizara zilikuwa zimeagizwa kutenga asilimia 2 ya bajeti zake kwa ajili ya kutengeneza nafasi za ajira.

'Vijana wanahitaji msaada'

"Ukosefu mkubwa wa ajira umesababishwa na kubadilika kwa mitazamo ya kibiashara duniani, Marekani kusitisha misaada ya kigeni, na kuongezwa kwa ushuru. Vijana wanahitaji msaada," Waziri Mkuu Sam Matekane alisema mwezi uliopita.

Waziri wa fedha wa Lesotho alisema mwezi Februari kuwa asilimia 38 ya vijana wa nchi hiyo hawana ajira.

Wanategemea zaidi kiwanda cha nguo

Nchi hiyo ambayo haina bandari, inategemea zaidi kuuza nguo nje ya nchi, nyingi ya hizo ilikuwa kwa soko la Marekani ambapo walikuwa wanasafirisha kwa makubaliano ya kutolipa ushuru wowote chini ya mpango wa AGOA.

Lakini nchi hiyo iliathirika zaidi Trump alipotangaza kuongeza kwa ushuru huku taifa hilo likiwekewa ushuru wa asilimia 50 – kabla ya agizo hilo kusitishwa.

Serikali imeonya kuwa huenda ikapoteza ajira hadi 40,000 kama makubaliano ya AGOA hayatasainiwa upya kufikia mwisho wa mwezi wa Septemba.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us