Akiwa amechoka, mjamzito na mwenye njaa, Nyandow Wie Deng na familia yake wanasubiri chakula katika kituo cha misaada katika mji ulio mpakani wa Muon katika eneo la Gambella nchini Ethiopia.
Wameacha kila kitu nyumbani Sudan Kusini, wakikimbia ghasia katika Jimbo la Upper Nile.
"Safari kutoka eneo la Nasir ilinichukua siku nne. Sikuweza kutembea haraka kwa sababu nilikuwa mjamzito,” anaelezea.
“Nilikuwa na uchungu mwingi, lakini ilinibidi kuvumilia kwa ajili ya watoto wangu. Ilinisumbua sana kuwaona bila chakula. Nilijaribu kukusanya kuni ili kuuza, lakini hali ilikuwa ngumu sana kiasi kwamba mimi na watoto wangu tuliumwa na mimi kukaribia kupoteza ujauzito wangu,” anaongeza.
Mama huyo ni mmoja ya waomba hifadhi 50,000 kutoka Sudan Kusini ambao wamevuka mpaka na kuingia nchini Ethiopia, wakitegemea kupata msaada wa chakula kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Licha ya kutimiza miaka 14, bado taifa hilo changa ulimwenguni halijapata amani na ustawi ambao uliahidiwa na Rais Salva Kiir wakati nchi hiyo ikijipitia uhuru, Julai 9, 2011.
Machafuko makubwa yaliibuka ndani ya Sudan Kusini, Disemba 2013 baada ya mvutano mkubwa kati ya Rais Kiir na Makamu wake wa Riek Machar.
Inakadiriwa kuwa watu wapatao milioni 2.3 walikimbilia nchi jirani, huku wengine milioni 2.23 wakilazimika kuyahama makazi yao kufuatia vurugu hizo za kisiasa.
Miaka 14 baada yake waliokimbilia nchi jirani ya Sudan wanalazimika sasa kurejea nchini mwao ambapo usalama bado ni shida, huku Sudan nayo ikijipata katika vita tangu Aprili 2023.
Mkataba dhaifu wa amani
Mkataba dhaifu wa amani wa 2018 ulifikiwa na Rais Salva Kiir, Riek Machar na vikundi vyngine ambavyo vilikuwa vikipigana.
Serikali ya mpito iliundwa kwa madhumuni ya kufanya uchaguzi ambao umeahirishwa mara kadhaa, ikiwa mipango ya Rais wa nchi ni kuchagua viongozi 2025 ulisimaishwa kwa madai kuwa serikali haikuwa tayari kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Mkataba huu ulifaa kuongoza kuundwa pia kwa majeshi ya pamoja, mifumo ya kisheria , na katiba ya kuongoza nchi hiyo.
Lakini miaka saba baadaye makubaliano hayo yanakabiliwa na changamoto za utekelezaji huku kukiwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar amewekwa katika kizuizi cha nyumbani huko Juba tangu Machi 2025 kutokana na mivutano ya kisiasa.
Uchumi wa nchi uko katika hali mbaya kwani vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu vimezuia mipango ya maendeleo.
Serikali inathibitisha kuwa asilimia 92 ya watu wanaishi katika umaskini na uhaba mkubwa wa chakula.
Utegemezi mkubwa wa mapato ya mafuta umeiacha katika hatari ya kuyumba kiuchumi.
"Nilifahamishwa kuwa hakutakuwa na sherehe rasmi kutokana na hali ya uchumi inayoendelea ambayo nchi imekuwa ikikabili. Kwa hivyo, hakuna sherehe zinazofadhiliwa na serikali," msemaji wa jeshi Meja Jenerali Lul Ruai Koang amewaambia waandishi wa habari.
Serikali inasema haina pesa ya raia kufanya sherehe za umma.
Huu ni mwaka wa 11 mfululizo bila matukio rasmi ya Siku ya Uhuru.
"Watu wanaweza kusherehekea faragha, au kwa vikundi ikiwa wanaweza kufanya hivyo," Lul alisema.
Barabara ya amani Sudan Kusini
Juhudi kadhaa za ngazi ya juu za kisiasa na kidiplomasia za IGAD, AU, Umoja wa Mataifa na Washirika wa Kimataifa hazijazaa matokeo madhubuti ili kutuliza mzozo wa kisiasa uliopo nchini humo.
Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Amani Sudan Kusini ( RJMEC) iliundwa na Shirika la Kikanda la IGAD kufuatilia makubalino ya amani ya 2018.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Juni 2025, Mwenyekiti wa RJMEC, Balozi Meja Jenerali George Owinow alionyesha hofu kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini humo.
"Hali ya sasa nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota, huku usitishaji mapigano wa kudumu ukidhoofishwa sana na Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Migogoro katika Jamhuri ya Sudan Kusini (R-ARCSS) ukiwa hatarini," alisema.
"Hali hii, ikiwa itaachwa bila kutatuliwa, ina uwezo wa kudhoofisha zaidi uaminifu na imani, uwiano wa kitaifa na maridhiano, na hivyo kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka sita iliyopita ya utekelezaji wa Mkataba wa Amani."
Akirejelea lengo la nchi hiyo kufanya uchaguzi Disemba 2026, Mwenyekiti wa RJMEC alisema kwamba kuna haja ya dharura ya kushughulikia changamoto ya sasa ya kisiasa "na kisha kuanza mchakato unaoharakishwa wa uundaji wa katiba, kuunganisha vikundi vya kisiasa na kujiandaa kwa uchaguzi ufaao."
Bado kuna imani ya mabadiliko
Licha ya kutokuwa na uongozi waliotarajia tangu 2011, wananchi wa Sudan Kusini wameonyesha imani yao kwa nchi yao hasa katika mitandao za kijamii.
“Tunaweza kuhisi tumesalitiwa na viongozi kuharibu tulichopigania, lakini angalau tuna nchi tunayoita yetu. Tunakumbuka damu, machozi na ujasiri uliotuweka huru. Alfajiri mpya itakuja. Tusikate tamaa,” @emmanuel_woja amesema katika X.
Umoja wa Afrika nayo umeonyesha imani yake kwa nchi hiyo.
“Siku hii inaashiria hatua muhimu katika safari ya Sudan Kusini kuelekea uhuru, umoja na ujenzi wa taifa. Umoja wa Afrika unapongeza uthabiti na azma ya watu wa Sudan Kusini na kusimama katika mshikamano na matarajio yao ya amani, utulivu na maendeleo. Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf amesema katika taarifa.
“Umoja wa Afrika unasalia na nia thabiti ya kufanya kazi bega kwa bega na Sudan Kusini ili kuendeleza ushirikiano wa kikanda, kukuza maendeleo endelevu, na kudumisha maadili ya pamoja ya Uafrika na umoja,” Youssouf ameongezea.