Andre Onana ataanza kwenye mechi ya Manchester United ya Ligi ya Europa dhidi ya Lyon siku ya Alhamisi, kocha Ruben Amorim amethibitisha.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon alifanya makosa mawili yaliyoisababishia timu yake kupata sare 2-2 nchini Ufaransa katika mechi ya robo fainali ya kwanza na akaachwa nje kwenye mechi yao ya ligi kuu ya England siku ya Jumapili ambapo walifungwa magoli 4-1 na Newcastle.
Mlinda mlango Altay Bayindir alicheza kwenye mechi hiyo katika uwanja wa St James' Park lakini Onana atarejea golini Old Trafford.
"Onana, atacheza kesho," Amorim alisema katika mkutano na waandishi wa habari.
‘Kuwasimamia wachezaji’
Kocha huyo raia wa Ureno anasema: "Kama kocha na mchezaji wa zamani kwanza najaribu kufanya mambo ambayo yatamsaidia mchezaji akiwa katika hali hii.
"Tunazungumzia kuhusu kuwasimamia wachezaji kwa afya zao lakini pia kuhakikisha wako sawa kiakili.
"Kulikuwa na wikiendi moja ambayo nilidhani tusingemchezesha Andre Onana na ingekuwa jambo jema kumpa nafasi Altay (Bayindir)."
Kocha huyo wa United pia amethibitsiha kuwa mshambuliaji Joshua Zirkzee hatokuwepo.
Zirkzee nje
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 23, aliondoka uwanjani akiwa anachechemea katika kipindi cha pili cha mechi yao ya Jumapili ambapo walishindwa.
"Joshua hatokuwepo tena msimu wote huu," alisema.
"Hatocheza tena msimu huu, acha tumuandae kwa msimu ujao.
"Ni ngumu kwake hasa wakati huu. Anajaribu kujiimarisha katika kila njia na ni vigumu kwa mchezaji yeyote."
Historia mbaya zaidi
United iko katika nafasi ya aibu sana kwenye ligi kuu ya England ikiwa nafasi ya 14 kwenye jedwali na wamebakisha mechi sita tu na inawezekana wakamaliza nafasi ya 17, ikiwa ni moja tu juu ya timu zinazoshushwa daraja.
Hii itakuwa nafasi mbaya zaidi ya kumaliza msimu tangu waliposhushwa daraja kutoka ligi kuu kwenye msimu wa 1973/74.
Lakini Amorim bado ana nafasi ya kumaliza misukosuko ya United kwa kuwaletea taji la Ulaya, ambalo huenda likaleta mabadiliko muhimu wakati akijenga timu upya.