Misri, Algeria na Nigeria zina majeshi yenye nguvu zaidi barani Afrika kufikia Juni 2025, hii ni kulingana na ripoti ya Global Firepower Index ya 2025.
Ripoti hiyo inatathmini majeshi ya nchi mbalimbali kwa kuzingatia idadi ya wanajeshi, kiwango cha mafunzo yao, na uwezo wa anga, ikiwa ni pamoja na idadi ya ndege za kivita na mifumo ya anga.
Kigezo kingine kinachotumika kupima nguvu za majeshi ni uwezo wao wa ulinzi ardhini. Katika kipengele hiki, magari ya kijeshi, vifaru, mizinga ya kuvutwa na virusha makombora pia hutathminiwa.

Kwa nchi zenye maeneo makubwa ya maji, nguvu za majini pia hupimwa. Katika kipengele hiki, idadi ya meli za kivita, manowari, vyombo vya doria za maji na teknolojia nyingine za majini huzingatiwa.
Nafasi ya kiuchumi ya nchi pamoja na mgao wa bajeti kwa majeshi ni kipengee kingine kilichotajwa na ripoti ya Global Firepower kama kigezo cha kupima nguvu za majeshi barani Afrika.
1. Misri
Misri, ambayo ina jeshi lenye nguvu zaidi barani, ina wanajeshi milioni 1.2, ambapo 440,000 hushiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi.
Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini yenye idadi ya watu milioni 115 ina wanajeshi 685,000 walioko katika jeshi la nchi kavu, 50,000 katika jeshi la anga, na 32,500 katika jeshi la majini.
Pia ina wanajeshi wa akiba wapatao 480,000 na vikosi vya ‘paramilitary’ iliyo na wanajeshi 300,000.
Jeshi la Misri lina zaidi ya magari 41,000 ya operesheni za ardhini, zaidi ya vifaru 3,600, mizinga inayojisukuma yenyewe zaidi ya 1,000, na takriban mizinga inayovutwa 960.
Katika jeshi la anga, Misri ina zaidi ya ndege 1,000, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita 238, helikopta 348, na ndege 354 za mafunzo.
Katika jeshi la majini, nguvu za kijeshi za Afrika zina vifaa vingi, ikiwa ni pamoja na manowari nane na meli mbili za kubeba helikopta zinazoweza kubeba mizigo ya tani 236,000.
2. Algeria
Algeria, ambayo inashika nafasi ya pili barani Afrika, ina jumla ya wanajeshi 610,000, ambapo 325,000 wanashiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi.
Jeshi la Algeria lina wanajeshi 182,500 wa nchi kavu, 14,000 wa jeshi la anga, na 6,000 wa jeshi la majini. Pia lina vikosi vya ‘paramilitary’ wapatao 150,000.
Algeria ina magari ya kijeshi 26,000, vifaru karibu 1,500, mizinga inayojisukuma 224, na mizinga inayovutwa zaidi ya 480.
Algeria ina jumla ya ndege 608 za kijeshi, zikiwemo ndege 102 za kivita, ndege 87 za mafunzo, helikopta 299 na ndege 10 za misheni maalum.
3. Nigeria
Nigeria, ambayo inashika nafasi ya tatu, ina jumla ya wanajeshi 280,000, ambapo 230,000 wanashiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi.
Jeshi la Nigeria lina wanajeshi 65,000 wa nchi kavu, 15,000 wa jeshi la anga, na 5,500 wa jeshi la majini. Pia lina vikosi vya ‘paramilitary’ wapatao 50,000.
Katika ardhi, Nigeria ina magari ya kijeshi 8,962, Vifaru 330, mizinga inayojisukuma 40, na mizinga inayovutwa 339.
Katika anga, Nigeria ina ndege 163, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita 14, helikopta 66, ndege maalum 11, na ndege za mafunzo 28.
4. Afrika Kusini
Afrika Kusini, ambayo inashika nafasi ya nne, ina wanajeshi 151,000, ambapo karibu nusu yao wanashiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi.
Jeshi la Afrika Kusini lina wanajeshi 62,800 wa nchi kavu, 13,815 wa jeshi la anga, na karibu 7,900 wa jeshi la majini. Pia lina vikosi vya ‘paramilitary’ wapatao 50,000.
Kwenye nchi kavu, Afrika Kusini ina magari 18,692 ya kijeshi, vifaru 252, mizinga inayojiendesha yenyewe, mizinga 134 ya kukokotwa na mizinga 101 ya roketi.
Katika jeshi lake la anga, nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 63, ina jumla ya ndege 182, zikiwemo helikopta 87, ndege za mafunzo 81 na ndege mbili za kivita.
Jeshi la wanamaji la Afrika Kusini lina nyambizi tatu na meli 33 za doria.
5. Ethiopia
Ethiopia inashika nafasi ya tano, ikiwa na jumla ya wanajeshi 162,000. Jeshi la nchi kavu lina wanajeshi 75,000, jeshi la majini lina 10,000, na jeshi la anga lina 5,000.
Katika nchi kavu, Ethiopia ina karibu magari 7,300 ya kijeshi, vifaru 338, mizinga 35 ya kujiendesha yenyewe, mizinga 309 ya kukokotwa na mizinga 40 ya roketi.
Katika jeshi lake la anga, Ethiopia, nchi yenye watu milioni 129, ina jumla ya ndege 103, zikiwemo helikopta 33, ndege za mafunzo 34 na ndege 25 za kivita.
Nchi nyengine za Afrika
Nchi nyengine zilizopenya katika nafasi za kumi bora ni Angola, Morocco, DRC, Sudan, na Libya.
Nchi nyengine ambazo majeshi yake yamejumuishwa katika 20 bora barani Afrika ni Kenya, Chad, Msumbiji, Tunisia, Tanzania, Cameroon, Côte d'Ivoire, Mali, Zambia na Ghana kwa mpangilio huo.
Miongoni mwa mataifa yenye viwango vya chini vya kijeshi barani Afrika ni Benin, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Sierra Leone na Liberia.
Orodha ya majeshi barani kwa viwango vyao vya nguvu
Ifuatayo ni orodha ya vikosi vya kijeshi barani Afrika, kutoka vikosi vyenye nguvu zaidi hadi vilivyo na nguvu kidogo, kulingana na takwimu ya Global Firepower Index ya 2025:
Misri
Algeria
Nigeria
Afrika Kusini
Ethiopia
Angola
Morocco
DRC
Sudan
Libya
Kenya
Chad
Msumbiji
Tunisia
Tanzania
Cameroon
Côte d’Ivoire
Mali
Zambia
Ghana
Zimbabwe
Sudan Kusini
Uganda
Namibia
Niger
Eritrea
Jamhuri ya Congo
Botswana
Mauritania
Senegal
Burkina Faso
Madagascar
Gabon
Liberia
Sierra Leone
Somalia
Jamhuri ya Afrika ya Kati
Benin
'Tathmini isiyo na upendeleo' ya nguvu za kijeshi
Global Firepower, ambayo hufuatilia taarifa zinazohusiana na ulinzi za nchi 145 kote duniani, inasema kwamba wao "hutumia zaidi ya vipengee 60 katika fomula yetu ya ndani ili kubainisha nguvu ya taifa husika."
Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani linasema pia kwamba orodha yake "inaruhusu mataifa madogo, yaliyoendelea zaidi kiteknolojia kushindana na mataifa makubwa, lakini yenye maendeleo duni."
Ili kusawazisha orodha hiyo, Global Firepower inasema: "Baadhi ya bonasi na adhabu huongezwa kwa uboreshaji ambao, mwishowe, tunatumai utawasilisha mtazamo usio na upendeleo katika uwezo wa kijeshi wa serikali."
Barani Afrika, Shirika la Global Firepower lilichambua nchi 38 kati ya 54 za bara hilo, bila maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu kuachwa nje ya orodha kwa nchi 16, ikiwa ni pamoja na Gambia, Togo na Malawi.