Kenya: Hatma ya maandamano ya Gen Z, mwaka mmoja baadaye
AFRIKA
5 dk kusoma
Kenya: Hatma ya maandamano ya Gen Z, mwaka mmoja baadayeLicha ya jitahada na ahadi za kuleta mabadiliko, serikali ya Kenya bado inaendelea kukuna kichwa, baada ya rika la Gen Z, kuazimia kufanya mandamano mengine makubwa Juni 25, 2025, kupinga yale yale ambayo waliyoyapinga mwaka jana.
Vijana nchini kenya wamepanga maandamano ya amani 25 Juni 2025 / picha : Reuters
23 Juni 2025

Kenya iko katika hali ya tahadhari huku vijana wakiapa kuingia barabarani Juni 25, 2025 kwa ajili ya maandamano ya amani.

“Nimesisitiza kwamba hakutakuwa na maandamano mnamo Juni 25, na siku hiyo itakuwa siku ya kawaida na yeyote anayetaka kuadhimisha siku hiyo ana uhuru wa kufanya maadhimisho nyumbani kwake,” alisema Isaac Mwaura, msemaji wa serikali ya nchi hiyo katika mahojiano yake ya Juni 23, 2025.

Hata hivyo, yumkini, maneno ya Mwaura hayana uzito kwa sasa, ikizingatiwa kuwa, makundi ya vijana nchini humo yamenuia kufanya maandamano siku hiyo.

Wengi wao wanasisitiza kuwa watatumia maandamano hayo, kuwaenzi wenzao wapato 60, waliouwawa na polisi wakati wakiandamana.

Itakapofika Juni 25 mwaka huu, itakuwa imetimia mwaka mmoja toka yatokee maandamano ya kihistoria nchini humo.

Mwaka jana, vijana kutoka kila pembe ya nchi hiyo, waliingia mitaani, kuupinga Muswada maalum wa Fedha 2024, lakini pia mfumo mzima wa uongozi, ambao waliutuhumu kuwa wa kibaguzi, kifisadi na kutojali masilahi ya wakenya.

Juni 25, wabunge waliokuwa wakijadili muswada huo, walipigwa na bumbuwazi, baada ya vijana wenye hasira kuvamia bunge hilo na kufanya uharibifu.

Mwaka mmoja baadaye, vijana nchini humo wanapanga kufanya maandamano dhidi ya serikali, pia wakiwaenzi wenzao waliopoteza maisha wakati huo.

Takwimu za Shirika la Haki za Binadanu la Kenya zinabainisha kuwa takriban watu 60 walifariki dunia kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano hayo.

Kilio cha familia za waliopoteza maisha

Katika tukio lililoacha wengi vinywa wazi, Juni 25, 2024, kundi la vijana lilivamia ukumbi wa bunge la nchi hiyo, wakati wa mjadala wa muswada huo tata.

Kati yao ilikuwa ni Kennedy Onyango, ambaye alipigwa risasi na polisi.

Kifo cha Kennedy bado kinaombolezwa na mama yake, mwaka mmoja baadaye.

“Kennedy Onyango alikuwa tumaini langu, lakini kwa sasa Mungu atabaki kuwa tumaini langu kwa sababu sioni haki yoyote ikipatikana,” alisema mama huyo wakati wa hafla iliyoandaliwa kwa wazazi waliopoteza watoto wao katika maandamano ya 2025.

“Mama huyu anasema alipokea simu kutoka kwa rais na akaongea naye, akimuahidi kuwa atamuita katika mkutano ili haki ya mwanaye, ipatikane.

“Rais aliniambia nitakufanyia vile mimi ningetarajia kufanyiwa kama mzazi, nawaambia ni mwaka mmoja sasa hakuna kilichofanyika,” anasema huku akifuta machozi.

Asubuhi ya Juni 25, 2024 , kijana mwingine Peter Macharia aliondoka kwao nyumbani Kibera, kitongoji katika mji mkuu Nairobi, kwenda kuungana na vijana wenzake kudai haki zao kwa serikali.

Mama yake hakuwahi kumwona tena.

Akiwa anamtafuta alienda katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta, ambapo alipata hati zinazoonyesha kwamba Peter alikuwa akitibiwa jeraha la risasi lakini hakukuwa na dalili yake kwenye chumba cha wagonjwa.

Mama yake hajawahi kumuona, hajawahi kumsikia kwa mwaka mmoja sasa.

"Walisema alikuwa ameruhusiwa kuondoka, lakini namjua mwanangu. Angeniita. Hakutoka nje," anaviambia vyombo vya habari.

Rose Ihoha naye anasema mtoto wake wa miaka 17, Austin Onyisa alipigwa risasi wakati wa maandamano katika mji wa Nakuru.

“Kumbe mtoto wangu alipigwa risasi na alikuwa amepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na mimi sijui, ni uchungu sana,” Ihoha alisema.

“Rais wetu alipo ajue wazazi tunaumia, ni uchungu sana,” alisema huku akitokwa na machozi.

Vijana wanataka nini?

Vijana katika mitandao ya kijamii hasa wanaoonesha kutoridhishwa na serikali ya Rais William Ruto, mwaka mmoja baadaye. Kilio chao mwaka huu ni kile kile, kama ilivyokuwa mwaka jana.

“Sisi kama vijana na wale ambao tunajitokeza kukataa hali ya sasa tunataka nchi inayofanya kazi, elimu, afya, yaani maisha ya Mkenya wa kawaida yawe mazuri kwa mahitaji ya msingi,” Sophie Mugure anasema.

Hatuogopi kuwa barabarani watakuja na silaha zao, sisi tutakwenda na Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo, Rais William Ruto wa Kenya, alisalimu amri na kutii matakwa ya Gen Z mwaka 2024.

Alianza kwa kufuta baraza lake lote la mawaziri. Hata hivyo katika uteuzi upya mawaziri wengine walirejeshwa katika nyadhifa tofauti. 

Baadae akautupilia mbali Muswada wa Fedha 2024. 

Maandamano ya Juni 2025 yanapangwa huku kukiwa na sintofahamu ya kupitishwa kwa sheria mpya ya muswada wa fedha.

Vijana waliinyoshea vidole vya lawama huduma ya taifa ya polisi, kwa kuonyesha ukatili kwa waandamanaji, ambapo takriban watu 60 waliuawa katika maandamano.

Mpaka sasa kuna wengine wanadaiwa hawajulikana walipo. Hali hiyo, ilisababisha Mkuu wa Polisi Japhet Koome kujiuzulu. 

Hata hivyo, hatua hizo bado hazijaleta unafuu wowote kwenye huduma ya polisi, kwani bado inalaumiwa kwa mauaji na mateso ya wananchi. 

Maandamano ya 2024, maarufu kama maandamano ya Gen Z, yaliashiria mwamko mpya wa kisiasa nchini Kenya na uwezekano wa kuleta mabadiliko bila kutumia majukwaa ya kisiasa.

Vijana ambao ndio idadi kubwa ya nchini humo, walionyesha kuwa inawezekana kuwapita walinzi wa jadi kama vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali, wafadhili wa kigeni na kuhamasisha haki za kiuchumi na utu kama wananchi tu. 

Serikali ya Rais Ruto imesisitiza kuwa inaweka sera za kuleta maisha bora kwa Mkenya ikiwemo kuanzisha mradi wa nyumba za bei nafuu kwa Wakenya.

Hata hivyo, licha ya jitahada za kuleta mabadiliko, serikali bado imejipata tena ikikabiliana na Gen Z ambao wanapanga tena kufanya maandamano makubwa Juni 25, 2025 kupinga yale yale ambayo waliyoyapinga mwaka jana.

 Rais Ruto anaendelea kukabiliwa na ukosoaji, haswa juu ya jinsi serikali yake inavyoshughulikia mauaji ya kiholela na ukiukaji wa haki za binadamu. 

Kwa upande wake, Rais Ruto ameendelea kujitetea na kusema kuwa anatekeleza majukumu yake kwa manufaa ya wananchi wake.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us