Masaibu ya raia mashariki mwa DRC
AFRIKA
3 dk kusoma
Masaibu ya raia mashariki mwa DRCMaelfu ya raia wa Congo wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mgogoro unaoendelea mashariki mwa Goma.
Wanawake wakifua katika Mto Kihiran katika eneo la Sake, karibu na Goma / REUTERS
3 Aprili 2025

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina idadi kubwa ya watu waliolazimishwa kuhama makazi yao, na hii ni matokeo ya miaka mingi ya mgogoro unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Baada ya kundi la wapiganaji wenye silaha la M23 kuendelea kushika udhibiti wa baadhi ya maeneo ya mashariki, kambi nyingi zilizokuwa zimehifadhi watu waliokosa makazi zimeharibiwa, hivyo maelfu ya wakimbizi wa ndani wamelazimika kutawanyika katika maeneo mbalimbali bila kujua hatma ya usalama wao ikoje.

M23 inasema hivi sasa ni salama kwa watu kurudi katika makazi yao, lakini kwa upande wake, UN inasema hii ni sawa na kuwalazimisha watu kukosa makazi. 

Marian Sandabi, ni mmoja wa raia wa Congo waliokuwa wakipata hifadhi katika kambi hizo mashariki mwa DRC. Hivi sasa amerudi nyumbani baada ya miaka kadhaa. Lakini hilo halikuwa chaguo lake.

Marian anasema kuwa amelazimika kurudi kwa sababu hawakuruhusiwa na kundi la M23.

“Imekuwa vigumu kurudi hapa. Tunahangaika kutafuta chakula na hakuna wa kutusaidia. Hasa watoto wanapata taabu,” Marian amemsimulia Rahul Radhakrishnan mwandishi wa TRT pindi alipokuwa Goma.

Vikundi vya wapiganaji wa M23 vinatuhumiwa kuwalazimisha watu waliokosa makazi kuondoka katika kambi zilizopo maeneo ya Goma na kuwataka warudi katika maeneo ambayo yamekuwa chini ya udhitibi wao mapema mwaka huu.

Hata hivyo, M23 imekana tuhuma hizo, na kusema kuwa watu wamerudi kwa hiyari yao. Lakini baadhi ya wachambuzi wanaiona hatua hiyo ya M23 ya kuwalazimisha raia kurudi katika maeneo yao ya awali, kama njia ya kujipatia umaarufu wa kisiasa baada ya kudhibiti maeneo hayo.

Buhoro Amani Veronique, ambae pia ni miongoni mwa waliokosa makazi, anasema, "Tulipewa siku tatu kubomoa vibanda vyetu. Walitutisha kutuchoma na vibanda vyetu iwapo hatutaondoka, kwa hiyo haraka tulivibomoa. Waliokataa vibanda vyao vilibomolewa. Ndani ya muda mfupi kambi ilikuwa tupu."

Ubomoaji wa kambi kwa lazima ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Hata hivyo, katika eneo hilo, hakuna sheria inayoonekana kufanya kazi.

Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na uhakika mdogo wa usalama, huku wengi wao wakikosa pa kwenda.

Amani Bwaraburiza Frederic, raia mwengine aliyekuwa kambini anakumbuka msaada watakaoukosa hasa baada ya kuondoka kambini.

“Awali, angalau msaada ulikuwa unatufikia, na madaktari walikuwepo kututibu. Maji pia yalikuwa ni rahisi kupatikana. Tulipata msaada. Lakini hivi sasa? Kila kitu kimebadilika na hatupati kitu tena,” anasema Amani.

DRC imekuwa katika mgogoro kwa miongo kadhaa sasa. Takriban watu milioni 4 wanaendelea kukosa makazi katika mikoa ya mashariki.

Natalia Torrent Martinez, Mkuu wa kutoka Shirika la MSF-Holland Goma Mission anasema kuwa hofu yake ni kwamba raia hawa ambao wameambiwa waondoke kambini, hawajui huko wanapokwenda hali itakuaje.

“Walikuwa wakipata misaada ya chakula, maji safi, matibabu, elimu na kila kitu,” anasema Natalia.

Makubaliano ya amani ya awali ya kumaliza mgogoro uliopo mashariki mwa DRC kati ya Serikali na vikosi vya M23 utekelezaji wake haujafanikiwa, huku pande zote zinazozozana zikidai kuwa mapendekezo hayo hayakuwa na msingi wowote.

Kwa raia hawa, kila kukicha hofu inazidi kutanda juu ya usalama wao na familia zao.

Julienne Kamundu Zawadi anasema, "Sina hakika kama watoto wangu wataishi vizuri. Sina hakika."

Kwa raia wa Congo ambao bado wanaandamwa na jinamizi la siku zilizopita, kusalimika katika kipindi cha sasa inazidi kuwa ngumu.

Tumaini pekee lililopo hivi sasa, ni iwapo jitihada zinazofanywa na jumuia za kikanda na kimataifa za kumaliza mgogoro huo zitazaa matunda. Ni suala la kusubiri na kuona.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us