Uhamiaji wa nyumbu, maajabu ya dunia
MAISHA
2 min read
Uhamiaji wa nyumbu, maajabu ya duniaKila mwaka watu kutoka sehemu tofuati duniani huja kushuhudia uhamiaji wa nyumbu au wildebeest zaidi ya milioni 1.5 unaofanyika kati ya Tanzania na Kenya.
Nyumbu wanavuka mto / Reuters
29 Novemba 2024

Na Coletta Wanjohi

Je, unajua kwamba kanda ya Afrika Mashariki imebeba mojawapo ya maajabu saba ya dunia?

Kila mwaka watu kutoka sehemu tofuati duniani huja kushuhudia uhamiaji wa nyumbu au wildebeest zaidi ya milioni 1.5 unaofanyika kati ya Tanzania na Kenya.

Msafara huu ni kati ya Hifadhi ya Serengeti Tanzania hadi Masai Mara, Kenya.

Nyumbu anaweza kukuwa na kufikia hadi mita 2.4 kwa urefu na kuwa na uzito wa kilo 270.

Nyumbu wanapatikana kusini na mashariki mwa Afrika. Nyumbu wa kawaida huishi katika misitu minene na nyanda za mafuriko kusini mwa Afrika na sehemu za Kenya na Tanzania, huku nyumbu mweusi huishi Afrika Kusini, Lesotho, na Eswatini.

Hata hivyo, uhamiaji wao pia unahusisha wanyama wengine wanao andamana nao kama vile pundamilia na swala.

Uhamiaji wa nyumbu kwa kawaida hufanyika kati ya mwezi Julai na Septemba, ambapo wanatoka hifadhi ya taifa ya Masai mara upande wa kenya kutoka hifadhi ya Serengeti Tanzania wakivuka mto Mara.

Kati ya Oktoba na Novemba nyumbu wanaanza kufanya safari na kuvuka mto Mara tena kurudi Serengeti.

Kwa sasa kati ya Januari na Machi ni wakati wao wa kuzaa katika sehemu ya kusini ya Serengeti na kaskazini mwa eneo la hifadhi ya Ngorongoro, Tanzania.

Nyumbu hubeba mimba kwa kati ya miezi nane hadi nane na nusu. Inakadiriwa kuwa takriban nyumbu laki tano wanazaliwa kila msimu.

Na nyumbu ni mnyama pekee mwenye uwezo wa kujizuia kuzaa iwapo yupo katika mazingira hatarishi, kwake na kwa mtoto wake.

Kila mwaka, maelfu ya nyumbu hufa wakati wa uhamiaji, wengine wakiliwa na mamba katika mto Gurumeti na wengine wakisombwa na maji wanapovuka mto Mara.

Wengine huvamiwa na wanyama wengine.

Lakini bado kila mwaka nyumbu wengine lazima wapitie hatari hii tena kwani ni lazima wafanye uhamiaji huu kwa sababu ndio sehemu ya maisha yao .

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us