ULIMWENGU
2 dk kusoma
Tetemeko Myanmar laharibu maeneo ya kale
Tetemeko lenye ukubwa 7.7 katika kipimo cha Richter lililopiga Myanmar wiki iliyopita, na kuuwa zaidi ya watu 3,000 limesababisha hasara kubwa katika eneo la kihistoria na maeneo ya ibada ikiwemo mji wa kale wa Ava.
Tetemeko Myanmar laharibu maeneo ya kale
Athari ya tetemeko la ardhi Myanmar / Reuters
4 Aprili 2025

Tetemeko la ardhi lililopiga Myanmar Machi 28 na kuharibu mji wa Ava katika jimbo la Mandalay, na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya kihistoria ya pagodas na sehemu za ibada, hayo ni kwa mujibu wa mtandao wa Myanmar Now.

Tetemeko hilo pia limeua takriban watu 300 katika mji wa Tada-U, uliopo katikati mwa Myanmar kilomita 10 kutoka mji mkuu wa Mandalay.

Wakazi wanasema, miili bado iko kwenye vifusi.

Majengo yote na nyumba katika mji wa Tada-U yameharibiwa na tetemeko,” amenukuliwa mkazi mmoja.

Idadi ya vifo vitokanavyo na tetemeko hilo mpaka siku ya Alhamisi imefikia 3,085, huku 4,719 wakijeruhiwa, na 341 hawajulikana walipo, limesema jeshi, kwa mujibu wa Myanmar Now.

Nako nchi jirani ya Thailand takriban 22 wamefariki na 70 hawajulikani walipo baada ya jengo la ghorofa lililokuwa linajengwa kuporomoka, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Umma (Thai PBS).

Wakati huo huo, Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB) imesema Jumatano kuwa inaandaa msaada wa kiasi cha dola milioni 3 kusaidia watu wa Myanmar.

Fedha hizo zitasaidia kusambaza chakula na pesa taslimu, kuwawezesha manusura kununua vitu muhimu kama maji ya kunywa, dawa na vifaa vya ujenzi.

“Tumesikitishwa sana na athari zake kwa watu a Myanmar na tunachukua hatua za haraka kutoa msaada wa dharura,” amesema Winfried Wicklein, Mkurugenzi Mkuu wa benki ya ADB kwa eneo la Kusini mashariki mwa Asia.

Uingereza imetoa ahadi ya msaada wa dola milioni 12 kwa Myanmar, huku Australia na Marekani kila mmoja ikiahidi dola milioni 2. Mfumo wa Dharura wa Umoja wa Mataifa umeweka kiasi cha dola milioni 5.

Jumatano, Australia imetangaza kuongeza kiasi cha dola milioni 7 za misaada, huku Japan ikichangia dola milioni 6, na China dola miliono 13.8.

Nchi nyingi za Kusini Mashariki mwa Asia ikiwemo Malaysia, Singapore na Thailand, pia zimetuma watu kusaidia.

Alhamisi China ilitangaza kuweka kituo cha kwanza cha huduma ya dharura Myanmar.

“China imeweka kituo cha kwanza cha kimataifa kwa walioathirika na tetemeko, kutoa makazi ya dharura na huduma za afya kwa watu 900 waliokosa makazi,” ameandika katika ukurasa wake wa X msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Mao Ning.

CHANZO:REUTERS
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us