Mahakama nchini Kenya imemruhusu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, kuondoa kesi ya jinai dhidi ya mfanyabiashara Mkenya Koome Kirimi aliyeshtakiwa kwa kumlaghai raia wa Rwanda zaidi ya Sh400 milioni (takriban Rwf4.47 bilioni) iliyohusisha kampuni ya teknolojia.
Katika uamuzi uliotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Milimani, Ben Mark, mahakama hiyo iliona ombi la DPP la kutaka kufuta kesi hiyo lilikuwa na uhalali.
"Kwa hivyo ninamwachilia Kirimi chini ya Kifungu cha 202 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai (CPC)," alisema hakimu.
Wakili wa upande wa utetezi, Stanley Kangai, anayemwakilisha mshtakiwa, hakupinga maombi hayo, huku akiifahamisha mahakama kuwa kesi hiyo imeendelea kwa muda mrefu kutokana na mlalamikaji kushindwa kuendelea.
Kirimi, mkurugenzi wa zamani wa Stay Online Limited, alishtakiwa kwa kula njama na watu wengine ambao hawakuwa mahakamani kwa kosa la kumlaghai Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Desire Muhinyuza, $2,619,583.27 (takriban Sh400 milioni mwaka huo).
Alidaiwa kufanya kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Julai 10 na Oktoba 2023 jijini Nairobi.
Mfanyabiashara huyo pia alikabiliwa na mashtaka ya kuiba dola 100,000 (takriban Sh14.9 milioni) kutoka kwa kampuni ya Stay Online Limited - fedha ambazo alikuwa amekabidhiwa kwa ajili ya kulipa kodi ya kampuni hiyo.
Zaidi ya hayo, Kirimi alishtakiwa kwa kuingiza dola 100,000 za uongo kwenye akaunti yake ya dola iliyokuwa katika Benki ya Equity na kutoa taarifa za uongo kwa afisa wa polisi.
Aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh500,000 baada ya kushtakiwa Oktoba 17, 2023.