AFRIKA
3 dk kusoma
Wanafunzi wafanya mtihani mashariki mwa Congo licha ya hali tete ya usalama
Maafisa wa elimu wenyewe wamesindikiza makaratasi ya mtihani kutoka mji mkuu, Kinshasa, hadi katika eneo linalotawaliwa na waasi kufuatia makubaliano yasiyo ya kawaida kati ya serikali na waasi wa M23.
Wanafunzi wafanya mtihani mashariki mwa Congo licha ya hali tete ya usalama
Mwanafunzi akifanya mtihani wa taifa katika chuo cha Alfajiri, mjini Bukavu, Mkoa wa Kivu Kusini nchini DRC. / Reuters
6 Juni 2025

Maelfu ya wanafunzi wa shule za sekondari wamefanya mtihani wao wa kitaifa katika eneo linalotawaliwa na waasi la mashariki mwa Congo wiki hii, mipango migumu iliyohitaji ushirikiano usiokuwa wa kawaida kati ya serikali na waasi wa M23.

Waasi walidhibiti miji miwili mikubwa ya mashariki mwa Congo mapema mwaka huu na sasa wanaonesha kuwa wanaweza kusimamia mamlaka vizuri.

Viongozi wa Afrika pamoja na Marekani na Qatar wanajaribu kwa sasa kutafuta amani ambayo itamaliza mapigano yenye mzizi wake katika mauaji ya kimbari ya Rwanda miongo mitatu iliyopita.

Mitihani hiyo ya kitaifa, inayofanywa na wanafunzi katika nchi hiyo nzima ya Afrika ya kati wakitarajia kujiunga na chuo kikuu, ilianza siku ya Jumatatu na itaendelea hadi katikati mwa mwezi Juni.

‘Vituo vyote vya mtihani vimepata makaratasi’

Ili mtihani ufanyike mashariki mwa Congo kulihitaji maafisa wa elimu kusindikiza wenyewe mitihani hiyo kutoka mji mkuu wa Kinshasa hadi katika miji inayodhibitiwa na M23.

"Tulikuwa miongoni mwa wale waliokwenda kuchukua mitihani mjini Kinshasa," alisema Jean-Marie Mwayesi, afisa wa elimu wa mkoa wa Kivu Kusini, ambapo M23 wamedhibiti sehemu kubwa.

"Tunashkuru juhudi za pamoja za maafisa wetu na washirika, vituo vyote 111 vimefikiwa."

Serikali ya Rais Felix Tshisekedi ilitangaza mwezi uliopita kuwa inaondowa ada ya mitihani - ambayo kwa kawaida ni zaidi ya dola 40 - kwa wanafunzi katika mikoa ya Kaskazini na Kusini ya Kivu, wakitoa sababu kuwa ni ukosefu wa usalama.

Pamoja na kuwa M23 wamewahi kusema kuwa wanataka kuiondoa madarakani serikali ya Tshisekedi, kiongozi wa kundi hilo Bertrand Bisimwa ameiambia Reuters kwamba bado wanatambua Kinshasa kama wasimamizi wa mitihani ya kitaifa.

‘Elimu haihusiki na siasa’

"Kuwepo kwetu hapa mashariki ya nchi haimaanishi kuwa hii ni nchi tofauti," Bisimwa alisema.

"Elimu ya watoto wetu haina uhusiano wowote na siasa. Lazima ilindwe kutokana na muingiliano wowote wa kisiasa kwa sababu sote tunapambana kwa ajili ya maslahi ya watoto wetu na maisha yao yawe mazuri."

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishtumu M23 kwa kuwaua raia wakiwemo watoto - madai ambayo kundi hilo inakanusha.

Exauce Katete alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya mtihani katika shule moja mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu, ambao ulidhibitiwa na M23 mwezi Februari na ambapo hali ya usalama imekuwa mbaya tangu wakati huo ikiwemo makundi ya sungusungu.

"Naam, kuna usalama. Bado naona watu wachache nje, wakijaribu kuhakikisha kuwa tuko salama. Hakuna usumbufu, hakuna kelele, kila kitu kiko shwari," Katete alisema, akieleza kuhusu askari kanzu waliowekwa na M23 nje ya shule.

Mwayesi, afisa wa elimu eneo hilo, amesema kuwa kati ya wanafunzi 44,000 waliojisajili kwenye kanda yake, karibu 42,000 walijitokeza, kukiwa na dhana kuwa wengine huenda waliondolewa katika makazi yao kutokana na vita.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us