Kwanini 'kazi za pembeni' zimekuwa kitu cha kawaida kwa Wakenya wa pato la wastani
AFRIKA
4 dk kusoma
Kwanini 'kazi za pembeni' zimekuwa kitu cha kawaida kwa Wakenya wa pato la wastaniKwa mujibu wa ripoti ya Geopol iliyofanyia utafiti sekta ya biashara na ajira nchini Kenya, asilimia 71 ya Wakenya walio katika ajira wanafanya biashara za pembeni.
Kenya side hustledelea kufanya biashara za pembeni kujazilia nakisi katika mishahara yao / Picha: Reuters / TRT Afrika Swahili
10 Juni 2025

Na Dayo Yussuf

Kwa kila mzazi, matumaini ya kumlea mwanae na kumpa elimu bora, ni aweze kujitegemea katika siku za baadae na hata kumudu kuanzisha familia yake.

Wengi wa wazazi wa kizazi cha X, yaani wazazi wa kizazi cha millenials walioko sasa, kujitegemea huku kunaweza kufanikiwa kupitia ajira.

Wakati huo, ndipo nchi za Afrika nyingi zilikuwa zinatoka katika ukoloni na kuanza ujenzi na upanuzi wa viwanda vya kujitegemea.

Wakati huo, ajira zilikuwa nyingi, muhimu ilikuwa ni mtu kupata bora elimu na kuanza kazi.

Uchumi umepanda lakini mishahara bado

‘‘Namshukuru Mungu mimi nilisoma na hata kazi nilipata punde tu baada ya masomo,’’ anasema Dyko Mwinyi, mkaazi wa Nairobi.

‘‘Kazi yangu ilinitosha kwa miaka kadhaa ya kwanza, lakini uchumi ulibadilika. Mfumko wa bei ukapanda, nisingeweza kutegemea tena mshahara kukidhi mahitaji yangu,’’ anaambia TRT Afrika.

Mwinyi ni mwandishi na mtaalamu wa filamu. Amefanya kazi hii kwa zaidi ya miaka kumi na mbili, lakini anasema uchumi ulipanda, lakini mshahara haukuongezeka.

‘‘Ule mshahara nilioajiriwa nao, licha ya kuongezewa japo kitone hapa na pale baada ya miaka, haukulingana kabisa na kasi ya gharama ya maisha. Bajeti yangu ya mwezi miaka mitano iliyopita haiwezi hata kunitolea mahitaji muhimu sasa hivi. Ilinibidi nitafute njia ya kujipatia kipato la ziada. Ilinibidi nitafute ‘side hustle.’’’ anasema Mwinyi.

‘Side hustle’ ni neno maarufu sana miongoni mwa Wakenya. Linamaanisha biashara ya kando mbali na ajira ya kawaida mtu aliyonayo.

Sahau kula au kulala

Mwinyi anatayarisha vipindi vya televisheni wakati wa mchana, ila pembeni ameanzisha biashara ya kufuga kuku wa mayai na siku za wikendi, anafanya kazi ya kuchukua video za harusi na shughuli nyingine kwa malipo.

‘‘Yaani wakati mwingine naweza kuwa busy sana nasahau kama hata kula au kulala, lakini nikiitiwa kazi wikendi na ni siku yangu ya mapumziko kazini, siwezi kuikataa kwasa babu nitakula nini? Mshahara wangu wanilipia kodi ya nyumba tu jijini,’’ anaambia TRT Afrika.

Juliet Akinyi, ameajiriwa kufanya kazi ya kusafisha na kupika chai katika benki.

‘‘Mimi sina masomo sana, kwa hiyo kazi niliyoajiriwa, japo nashukuru sana, haina mshahara mkubwa,’’ anasema. ‘‘Lakini nikitoka kazi, huwa napitia nyumba kadhaa wananipa kazi ya kuwafulia nguo hasa wakati wa wikendi, na hapo napata pesa ya matumizi ya kila siku, nikujituma tu’’ anaongeza.

Kazi za kidijitali na mtandaoni

Kwa mujibu wa ripoti ya Geopol iliyofanyia utafiti sekta ya biashara na ajira nchini Kenya, asilimia 71 ya Wakenya walio katika ajira wanaendesha biashara za kando.

Walipoulizwa kuhusu mapato yao ya sasa ya mishahara, kundi kubwa zaidi, 44%, lilisema linapata chini ya Kes. 30,000. Hii inafuatwa na 20% wanaopata mapato kati ya Kes. 30,000 na Kes. 50,000, na kisha 17% ambao wana mapato kuanzia Kes. 50,000 kwa Kes. 80,000. Ni 6% pekee walisema wanapata mapato zaidi ya Kes. 150,000.

Wengi wao wanafanya ima kazi za mtandaoni, ambazo wanaweza kufanya wakiwa nyumbani, au biashara nyingine maarufu ni dereva wa uber, au kilimo na ufugaji. Baadhi pia walielezea kuwa na maduka ambapo wanaweza kuajiri mtu kumsimamia.

Mwinyi anasema biashara yake ya mayai imeanza kuleta tija na matumaini ya kukua zaidi.

Janga la Covid liliwafungua wengi macho

‘‘Mwanzoni ilikuwa tabu kukimbizana kutoka kazi moja hadi nyingine. Biashara ni uwekezaji na inahitaji uwe makini nayo wakati wote. lakini sasa nishazoea na nimeelewa namna ya kujipangia muda wangu. Nimeajiri vijana wawili wanaosimamia biashara zangu sasa. Pengine biashara ikifaulu nitaachana na ajira’’ anasema mwinyi.

Wakenya wanasifika kwa kujituma sana hasa katika kazi za kidijitali. Kwa mujibu wa ripoti ya Geopol, asili mia 87 ya Wakenya walionesha nia ya kuanzisha biashara zao binafsi, ima kando ya ajira au waachane na ajira kabisa.

Na kama ilivyokuwa katika maeneo mengi duniani, janga la Covid 19 lilisaidia kuwafungua wengi macho kwa talanta zilizofichika hasa katika ubunifu wa kidijitali.

Hii iliwasukuma baadhi kutoa fursa zaidi katika nyanja hiyo ili kujipatia riziki ya kando, na licha ya ofisi kufunguliwa na watu kurejea kazini kama kawaida, waliokuwa tayari wanapata shilingi kadhaa mtandaoni waliamua kuendelea.

Ajira sio mwisho

Serikali nayo pia inahimiza utamaduni wa kujituma hasa katika sekta binafsi, ili kuondoa mzigo wa ukosefu wa ajira.

Ripoti ya Geopol inasema kuwa, miongoni mwa watu waliotambuliwa kama wasio na ajira, ambao wanajumuisha 37% ya watu waliohojiwa, 91% kubwa wanatafuta kazi kwa bidii.

Lakini ni wazi kwamba, safari ya kuongeza kipato haiishii katika kupata ajira, na kwa Wakenya wengi waliojairiwa, wako tayari kufanya kazi ya aina yoyote kuongezea kipato maishani mwao, wanasema ‘Side Hustle’ ni lazima.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us