Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mke wake, Janet, wamejisajili kwa ajili ya kupata vitambulisho vipya ambavyo vinatolewa na taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kwa mujibu ya sheria, taifa hilo linabadilisha vitambulisho vyake vya kitaifa baada ya kila miaka 10.
Vitambulisho vya sasa vilitolewa kati ya 2014 na 2015, lakini matumizi yake yaliongezwa kwa mwaka mmoja mwingine ili kutoa nafasi kwa raia kusajili upya.
Museveni ametoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kujisajili kwa vitambulisho hivyo vipya.
“Leo, Maama Janet (Mke wa Rais) na mimi tumesajili kwa ajili ya vitambulisho vipya huko Nakasero. Nawaomba raia wote wa Uganda ambao wamefikisha umri unaotakiwa wafanye hiyo ili waweze kupata huduma iliomarika,” alisema katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumanne.
Kitambulisho kimeimarishwa
Watu wanahitaji vitambulisho ili waweze kupata huduma za serikali na pia kusaidia kusafiri katika kanda hii. Vitambulisho vipya vimeimarishwa kiteknolojia ikiwemo kuunganishwa na taarifa binafsi za mtu.
Mwaka uliopita, nchi hiyo ilifanya sensa yake ya kwanza kidijitali.
Usajili wa vitambulisho vipya ulizinduliwa mwisho wa mwezi Mei na utaendelea kwa miezi 10 ijayo.
Wakati wa usajili, watu wanatakiwa kwenda na vitambulisho vyao vya zamani au barua ya polisi kama wamepoteza vitambulisho vya zamani.