Hungaria imetangaza mpango wa kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wakati ambapo Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, analitembelea taifa hilo.
Mahakama ya ICC inamtuhumu Netanyahu kwa kuhusika na uhalifu wa kivita huko Gaza.
Maamuzi ya Hungaria yanakuja wakati Waziri Mkuu wa nchi hiyo Viktor Orban akiwa mwenyeji wa Netanyahu, jijini Budapest, kwa ziara yake ya kwanza barani Ulaya toka mwaka 2023.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 huko The Hague nchini Uholanzi, mahakama ya ICC ina jukumu la kuwashitaki watu wanaohusika na uhalifu mkubwa, iwapo mataifa wanapotoka watu hao watashindwa kufanya hivyo.
"Ni muhimu kwa demokrasia. Ni muhimu kupingana na chombo hichi kilichojaa rushwa," alisema Netanyahu wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Orban.
Kwa upande wake, Orban aliituhumu ICC kwa kukiita “chombo cha kisiasa” chenye “kuonesha upendeleo."
Novemba mwaka jana, Orban alimkaribisha Netanyahu nchini Hungaria, siku moja baada ya ICC kutoa hati ya kukamatwa kwake.
Kulingana na Orban, Hungaria itaanza mchakato wa kujiondoa ICC siku ya Alhamisi.