Akiwa na umri wa miaka 21 tu, Jahleel Mollel, kijana wa kitanzania amejizoelea umaarufu mkubwa kwenye tasnia ya utengenezaji maudhui nchini Kenya.
Jahleel, ambaye maana ya jina lake ni “mtu anayemtegemea Mungu”, alipewa jina hilo na wazazi wake, ambao walivutiwa na mhusika Jaleel White au Steve Urkel ambaye alipata umarufu kwenye vichekesho vya ‘Family Matters’ kipindi hicho.
"Jaleel si mtu anayetajwa sana kwenye Biblia, lakini ndiye aliyefuata nyota. Hivyo, ni mtu aliyemtegemea Mungu kwa kila kitu,” anasema Mollel katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Kuvutiwa na sanaa ya vichekesho
Hata hivyo, utengenezaji maudhui haukuwa chaguo la kwanza kwa Mollel kwani alikuwa na ndoto za kusomea shahada Teknolojia ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Strathmore kwa lengo la kutafuta suluhu za changamoto za kibiashara kupitia teknolojia. Hata hivyo, Mungu alikuwa amempangia mengine.
Baada ya kumpoteza mdogo wake na kupitia changamoto za kiafya, Mollel akageukia utengenezaji maudhui kupitia jukwaa la TikTok.
Mang’amuzi binafsi
"Nilifiwa na mdogo wangu mara tu baada ya kujiunga na Chuo Kikuu. Nilitamani sana kutoa simulizi yangu," anasema.
Alianza kama mzaha tu, kumtumia mama yake kuhusu maisha yake ya chuoni nchini Kenya, bila kujua kuwa siku moja itakuwa sehemu ya kitu apendacho kufanya.
"Nilirekodi picha mbalimbali za video, kuhusu nilichokuwa nakula chuoni mimi na marafiki zangu na kumtumia mama yangu. Wanafunzi wenzangu walicheka sana."
Umaarufu na mikataba ya kazi
Umaarufu wake ulianza kupitia video zenye kuonesha watu wakiiba chaji za simu, hatua iliyomfanya kuanza kufanya vichekesho.
"Watu waliifurahia kwanini ilikuwa na mengi ya kuwahusu".
Hata hivyo, ilikuwa ni vigumu kwake kuanza kujijengea jina kutokana na kudhulumiwa kibiashara.
"Sikujua thamani yangu kwa wakati huo. Makampuni mbalimbali yalinijia na nilikubaliana nao tu bila kufahamu kile nilichotakiwa kuwatoza. Ila kwa sasa ninao uelewa, nadhani ni muhimu kwa watengeneza maudhui wapya wajengewe uelewa kwenye hili," anasema.
Uhalisia zaidi
Asilimia kubwa ya maudhui ya Mollel yameegemea uhalisia, huku akimalizia na kauli yake ya maarufu ya “Asante , Kwaheri".
"Kila anapochukia wakati wa mazungumzo yetu ya simu, mama hupenda kusema ‘Asante, kwaheri’, tena kwa sauti ya ukali, ndipo nami nikaamua kuchukua kama kibwagizo cha video zangu."
Hata hivyo, safari ya Mollel haikuwa rahisi, hasa macho yako yanapokutana na kovu lililotokana na upasuaji aliowahi kufanyiwa hapo awali..
"Ni muhimu kupuuzia maoni ya watu wasiojua umetoka wapi."
Kuacha alama
Huku akiweza kujigawa, kati ya masomo na utengenezaji maudhui, Mollel alielekeza nguvu zake katika kujijenga kitaaluma na kibunifu.
"Nataka ikifika mwaka 2027, mdogo wangu awe amemaliza shahada yake ya uzamivu ifikapoka mwaka 2027," anaiambia TRT Afrika.
Ushauri wake kwa watengeneza maudhui wajao?
"Wajijengee uthubutu wa kujaribu vitu vipya bila hofu yoyote. Ni muhimu sana kuwa na mwendelezo kwenye kile ukifanyacho."