AFRIKA
2 dk kusoma
CCM yaahirisha vikao vya kitaifa bila kutangaza tarehe mpya
Katika barua iliyosambazwa mitandaoni, katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama alielezea kwa ufupi tu kuwa ni kutokana na sababu za kiufundi.
CCM yaahirisha vikao vya kitaifa bila kutangaza tarehe mpya
Chama Cha Mapinduzi kimeshutumiwa kwa namna kimeteua wagombea / CCM - X / Others
19 Julai 2025

Chama Cha Mapinduzi nchini Tanzania kimetangaza kuahirisha vikao vyake vya kitaifa kutokana na kile kimetaja kuwa 'sababu za kiufundi'.

Vikao hivyo vilikuwa vimepangiwa kufanyika Julai 18 - 19 vikihusisha Kamati ya Usalama na Maadili pamoja na Kamati Kuu ya chama.

‘‘Nachukua fursa hii kuwajulisheni kuwa kutokana na sababu za kiufundi, vikao vya CCM vya kitaifa, vilivyopangwa kufanyika tarehe 18-19/07/25 (Kamati ya Usalama na Maadili - Kamati Kuu) sasa vimeahirishwa hadi hapo itakapotangazwa tarehe nyingine,’’ ilisema taarifa hiyo.

Kuahirishwa huku kunakuja wakati chama kipo katika mchakato muhimu wa kutathmini utekelezaji wa shughuli ya kisiasa na kiutawala kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Pia hatua hii inakuja siku moja baada ya mkutano na waandishi wa habari wa aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kukashifu uteuzi ulivyofanywa na chama wa wagombea wakuu, akisema 'CCM inatakiwa kuchagua viongozi wenye sifa'

Balozi Polepole alilalamikia pia mchakato wa kumchagua mgombea urais wa nchi hiyo uliofanyika Januari 2025.

Polepole alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake ya kidiplomasia na uongozi wa umma, akitaja kukosekana kwa uelekeo sahihi katika uongozi wa kitaifa, kufifia kwa maadili katika ngazi mbali mbali serikalini na kutoheshimiwa haki za raia.

Barua hiyo ya CCM iliyosainiwa na katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa, Salum Khatib Reja, haikutaja tarehe mpya ya vikao hivyo.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us