Makhosetive Dlamini, au mfalme Mswati wa III, kama anavyojulikana na wengi duniani, alizaliwa Aprili 19, 1968, huko Manzini.
Kwa sasa, ana wake 16 na watoto wanaokadiriwa kufikia 45.
Baba yake aliitwa Mfalme Sobhuza wa II na mama yake alikuwa ni Ntfombi Tfwala.
Mwaka 1986, alitawazwa kama Mfalme wa Swaziland, kufuatia kifo cha baba yake, na hivyo kuwa mtawala mwenye umri mdogo zaidi duniani katika karne ya 20, akichukua nafasi hiyo akiwa miaka 18 na siku 6 tu.
Akiwa kama mtawala wa Eswatini, Mfalme Mswati wa III ana mamlaka ya kumteua Waziri Mkuu wa himaya hiyo, baraza la mawaziri na wafanyakazi wa mahakama, japo hana uwezo wa kumchagua mrithi wake.
Hata hivyo, kulingana na madaraka yake, Mfalme Mswati wa III ana kinga ya kutokushitakiwa.
Katika utawala wake, Mfalme Mswati wa III ameitembelea Taiwan mara 17, na hata kuahidi kulitambua taifa hilo badala ya China.
Mwaka 2021, Mfalme Mswati wa III aliugua maradhi ya Uviko-19, na baadaye kuishukuru Taiwan kwa kufanikisha matibabu yake.
Mara kadhaa, mfalme huyo ametuhumiwa kuwateka wanawake kwa tamaa zake za kuoa.
Ikumbukwe kuwa, Mfalme Mswati wa III huchagua wake zake kupitia ngoma maalumu ya kijadi ambayo hufanyika kila mwaka.
Pia, amenyooshewa kidole kutokana na maisha yake ya kifahari huku wananchi wake wakiishi katika umasikini.
Kwa mfano, mwaka 2014, bunge la nchi hiyo liliidhinisha bajeti ya Dola za Kimarekani Milioni 61 kwa matumizi ya mfalme huyo, huku asilimia 70 ya raia wa Eswatini wakiishi kwa chini ya dola 1.25 kwa siku.
Alipiga marufuku upigwaji picha wa magari yake baada ya kutuhumiwa kuwa ananunua magari ya kifahari kama vile DaimlerChrysler Maybach 62.
Kulingana na jarida la Forbes, utajiri wa Mfalme Mswati wa III ulifikia dola milioni 500 kwa mwaka 2023.
Mwaka 2018, Mfalme Mswati alibadili jina la nchi hiyo kutoka Swaziland na kuwa Eswatini.
Nia yake ilikuwa ni kuondoka mkanganyiko na Switzerland, nchi inayopatikana katika mwa bara la Ulaya.