Michezo ya video na matatizo ya kusikia
Michezo ya video na matatizo ya kusikia
Wataalamu wa afya wanahofia kwamba michezo mingi ya kisasa ya video haina mifumo ya usalama ya kuwalinda watumiaji dhidi ya viwango vya sauti ya juu.
14 Machi 2025

Na Pauline Odhiambo

Sio siri kwamba kuzeeka mara nyingi huja na aina fulani ya udhaifu wa kusikia, lakini hivi karibuni kuna idadi inayoongezeka ya vijana wanaokabiliwa na matatizo ya kusikia, wataalam wa afya wanasema. Moja ya sababu kuu ni michezo ya video.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mamilioni ya wachezaji wenye umri mdogo duniani kote wako katika hatari ya kupoteza kabisa uwezo wa kusikis kutokana na kuathiriwa kwa muda mrefu na sauti kubwa wanapocheza michezo ya video au kusikiliza muziki.

Ripoti ya WHO ya 2025 inakadiria kuwa karibu watu bilioni tatu duniani kote hucheza michezo ya video kwenye vifaa kama vile kompyuta, na simu za rununu. Walakini, vifaa hivi vingi havina mifumo ya usalama iliyojengewa ndani ili kulinda watumiaji dhidi ya viwango vya sauti ya juu.

Shirika la afya duniani linaonya kwamba kufikia mwaka wa 2050, kulingana na makadirio takriban watu bilioni 2.5 duniani kote wana hatari ya kuwa na kiwango fulani cha udhaifu wa kusikia.

Watoto hatarini zaidi

Watoto wako kwenye hatari zaidi. Kutokana na uhimilivu wa chini wa miili yao kukabiliana na sauti kubwa, na pamoja na kupenda kwao sana michezo, jambo ambalo huwaweka katika hatari kubwa, huku baadhi ya wazazi wakijitahidi kuwadhibiti.

"Ninalazimika kuwakumbusha wanangu mara kwa mara kupunguza sauti wanapocheza," Ted Ouma, baba wa watoto watatu nchini Kenya anaiambia TRT Afrika.

"Imekuwa changamoto kuwafanya wacheze nje na watoto wengine kwa sababu wanapenda michezo ya video tu."

Hata hivyo matatizo haya hayakomi tu kwa watoto wa Ouma. Watoto wengi huvutiwa na madoido na nyimbo ambayo hufanya michezo ya video iwe ya kusisimua sana. Ingawa ripoti ya UNICEF ya 2024 iliangazia kwamba michezo ya video inaweza kusaidia ustawi wa watoto inapoundwa kwa kuzingatia mahitaji yao, hatari za kupoteza uwezo wa kusikia inayosababishwa na sauti ya juu, inasalia kuwa wasiwasi mkubwa.

Madhara ya sauti kubwa

Kuwepo kwa mifumo mingi inayotoa ufikiaji wa michezo ya mtandaoni, inarahisisha wachezaji, hasa watoto, kutumia saa nyingi kwenye skrini, kusikiliza kupitia spika, vipokea sauti vinavyovaliwa kichwani au vipokea sauti vya masikioni kwa sauti za juu.

Kupoteza uwezo wa kusikia mara nyingi huhusishwa na magonjwa, majeraha pamoja na kuzeeka. Takriban nusu ya watu wazima walio na umri wa miaka 70 na 80% ya walio na umri wa zaidi ya miaka 85 hupoteza uwezo wa kusikia.

Hata hivyo, miongozo ya WHO inasema kwamba watu wazima wengi wanaweza kuvumilia kwa usalama, kizio cha kiwango 80, takriban kiwango cha sauti ya kengele ya mlangoni, kwa hadi saa 40 kwa wiki. Zaidi ya hiyo, huwa ni hatari.

"Kwa watu wazima, kizio cha kiwango 90, ni salama kwa saa nne tu kwa wiki, na 95 kwa saa moja tu na dakika 15," anaelezea Jackline Mutua, daktari wa masikio, pua and koo (ENT) anayeishi Nairobi, anaiambia TRT Afrika. "Kwa watoto, viwango vya kizio ni chini sana."

Michezo ya sauti,matatizo kwa masikio

Utafiti wa 2024 uliochapishwa katika jarida la BMJ Public Health ulipima viwango vya sauti ya juu za vipokea sauti vinavyovaliwa kichwani katika michezo minne maarufu ya mapigano ya risasi, vikionyesha viwango vya kizio cha kati ya 88.5 na 91.2.

Kwa watoto, kizio cha sauti wa kinachoruhusiwa ni 75 kwa saa 40 kwa wiki. Hii ina maana kwamba watoto wanaweza kusikiliza kiwango cha kizio 83 kwa usalama, kwa takriban saa 6.5, kizio 86 kwa saa 3.25, kizio 92 kwa dakika 45, na kizio 98 kwa dakika 12 tu kila wiki.

Utafiti huo pia uligundua kuwa sauti za msukumo - milipuko mifupi, kubwa kama milio ya risasi - inaweza kufikia hadi kiwango cha kizio 119, na kusababisha uharibifu wa haraka kama vile kuwa kiziwi.

Wavulana, haswa, walionekana kucheza michezo ya video mara nyingi zaidi, kwa muda mrefu, na kwa viwango vya juu kuliko wasichana.

Wataalamu wanaonya kuwa idadi ya vijana inazidi kuathirika kutokana na kucheza kwa sauti kubwa.

"Sikio la ndani lina chembechembe ndogo za nywele ambazo hutusaidia kusikia kwa kuchukua mitetemo ya sauti," aeleza Dkt Mutua, ambaye huwatibu watoto.

"Kuzeeka kwa kawaida hupunguza seli hizi, lakini viwango vya juu vya sauti, kama zile za michezo ya video yenye sauti kubwa, pia inaweza kuziharibu kwa njia isiyoweza kurekebishwa," anaongeza.

Njia salama zaidi

Ingawa kucheza kwa sauti kubwa kunachangia sana, sababu zingine zinaweza kusababisha uwezo wa kusikia.

Magonjwa kama vile mabusha na uti wa mgongo, pamoja na baadhi ya dawa kama vile aspirini, kwinini na tiba kemikali, zinaweza kudhuru uwezo wa kusikia, wataalam wanaonya.

"Wachezaji wanaweza kupunguza sauti ili kupunguza hatari, lakini suala kuu ni muda wa kucheza, haswa kwa watoto," Dkt Mutua anaonya.

Ili kukabiliana na wasiwasi huu unaokua, Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) na WHO wametoa maagizo ya viwango vya kwanza vya kimataifa vya usikilizaji salama katika mchezo wa video. Iliyotolewa kufuatia Siku ya Usikivu Duniani mnamo Machi 3, viwango hivi vinalenga kuzuia upotezaji wa kusikia miongoni mwa wachezaji kwa kutoa maelezo, maonyo na vipengele vya usalama.

Miongozo inapendekeza:

Ufuatiliaji wa kiwango cha sauti: Hupima kiwango cha sauti ya mchezaji katika muda halisi.

Hali ya usalama ya vipokea sauti: Hurekebisha sauti kiotomatiki wakati wa kubadili kati ya vipokea sauti vya masikioni na spika.

Maonyo ya skrini: Ujumbe wa mara kwa mara hufahamisha wachezaji kuhusu matumizi ya sauti na kutabiri wakati vikomo vya usalama vitakiukwa.

Wazazi wanaweza kutumia vipengele hivi kuweka viwango vya sauti salama kwenye vifaa vya watoto wao, na hivyo kuhakikisha matumizi bora ya michezo ya video.

Kuchukua hatua

"Kila mtu anaweza kuchukua hatua leo kulinda masikio yake ," Dk. Jérôme Salomon, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO kwa Huduma ya Afya kwa Wote alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari inayoelezea viwango vya kimataifa vya usikilizaji salama.

"Kiwango cha usikilizaji salama cha WHO/ITU kinawezesha serikali, watengenezaji na mashirika ya kiraia kuunda mazingira salama ya usikilizaji, kuhakikisha kwamba watu wa rika zote wanaweza kufurahia shughuli kama vile michezo ya video bila kuhatarisha usikilizaji wao."

Hapo awali,hakuna miongozo ya kimataifa iliyokuwepo ya usikilizaji salama katika uchezaji wa video. Sasa, kukiwa na viwango hivi vipya, tumaini ni kusawazisha kati ya furaha ya kucheza michezo na kuhifadhi afya ya kusikia, hatua muhimu kwa mamilioni ya wachezaji wachanga ulimwenguni.

Kadiri tasnia ya michezo ya video inavyoendelea kukuwa, ndivyo pia lazima ufahamu wa hatari zake uwepo.

Kwa wazazi kama Ted Ouma, hatua hizi hutoa njia ya kulinda usikivu wa watoto wao bila kuwanyima michezo wanayopenda. Baada ya yote, sauti ya kicheko na kucheza haitakiwi kamwe kuzamishwa na ukimya wa upotevu wa kusikia unaoweza kuzuiwa.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us