Polisi wa Kenya waliwarushia vitoa machozi wanaharakati mara mbili walipokuwa wakiandamana hadi kituo kikuu cha polisi katika mji mkuu Nairobi wakati wa maandamano Jumatatu kupinga kifo cha mwanablogu chini ya ulinzi wa polisi chini ya hali isiyoeleweka.
Albert Ojwang alipatikana amekufa akiwa kizuizini katika Kituo Kikuu cha Polisi na polisi walihusisha kifo chake na "kugonga kichwa chake kwenye ukuta wa seli," lakini wanaharakati wamehoji sababu ya kifo hicho.
Ojwang alikamatwa Ijumaa huko Homa Bay magharibi mwa Kenya na kusafirishwa kilomita 400 (maili 248) hadi Nairobi kwa kile polisi walisema ni kuchapisha "taarifa za uwongo" kuhusu afisa mkuu wa polisi kwenye mitandao ya kijamii.
Kifo cha mwanablogu huyu kinakuja takriban mwaka mmoja baada ya wanaharakati na waandamanaji kadhaa kuuawa na kutekwa nyara na polisi wa Kenya wakati wa maandamano ya mswada wa fedha mwaka wa 2024.
Wengi wanatilia shaka
Mtafaruku wa kiuchumi bado uko juu, licha ya kodi iliyopendekezwa kutupiliwa mbali mwaka jana.
Polisi wa Kenya walisema Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi imeanzisha uchunguzi.
Maafisa waliokuwa zamu Ojwang alipofariki akiwa kizuizini pia hawatarejea kazini wakisubiri matokeo ya uchunguzi, alisema Inspekta-Jenerali wa polisi Douglas Kanja.
Hata hivyo, wengi wana mashaka na kesi hiyo.
Masuali mazito yaibuka
"Hadi sasa wao (Polisi wa Kenya) hawajatuambia ukweli. Tunajua kulikuwa na majeruhi zaidi. Wameamua kuwatoa mhanga maafisa wa chini. Tunataka haki kwa Ojwang na wengine wengi ambao wamepoteza maisha," alisema Hussein Khalid kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty Kenya lilisema kwenye taarifa kwamba kukamatwa kwa Ojwang kunazua maswali mazito na kwamba matokeo ya ripoti ya IPOA lazima yatangazwe kwa umma na maafisa wowote watakaopatikana na jukumu lazima wawajibishwe kikamilifu.
Kifo cha Ojwang kiliendelea kuzua ghadhabu mtandaoni na kimeibua upya wito wa maandamano ya kudai uwajibikaji kutoka kwa serikali.