AFRIKA
2 dk kusoma
Waporaji wasababisha hospitali ya mwisho Sudan Kusini kufungwa
Shirika la MSF linasema limesitisha usaidizi wake kutoka kwa vituo 13 vya afya katika jimbo la Upper Nile, likiongeza kuwa hatua hiyo sasa imefanya eneo hilo "kutokuwa na kituo chochote cha afya"
Waporaji wasababisha hospitali ya mwisho Sudan Kusini kufungwa
Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini limekumbwa na mapigano ya mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni. / Reuters
10 Juni 2025

Shirika la Madaktari wasiokuwa na mipaka (MSF) limesema Jumanne kuwa limelazimika kufunga hospitali Sudan Kusini baada ya uporaji kuzidi, na kuacha kaunti ndogo na inayokabiliwa na mapigano bila kituo chochote cha afya.

MSF inasema hospitali ya Ulang, katika jimbo la Upper Nile, "imeharibiwa kabisa" baada ya watu wenye silaha kuvamia kituo hicho mwezi Aprili, kutishia wahudumu na kupora dawa zenye thamani ya dola 150,000.

Uvamizi huo umefanya kituo hicho kuwa "katika hali mbaya na kushindwa kutoa huduma", lilisema katika taarifa.

Sudan Kusini imekuwa katika mapigano mengine katika miezi ya hivi karibuni kutokana na makubaliano ya kugawanya madaraka kati ya majenerali hasimu, Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, kutibuka.

‘Hamna njia nyingine’

"Hasara kubwa kutokana na uporaji imefanya sasa hatuna raslimali zozote muhimu kuendeleza huduma zetu. Hatuna njia nyingine ila kufanya maamuzi magumu ya kufunga hospitali hiyo," Mkuu wa ujumbe wa MSF nchini Sudan Kusini Zakaria Mwatia alisema.

MSF inasema imesitisha msaada wake kwa vituo 13 vya afya katika kaunti hiyo, akiongeza kuwa hali hiyo imefanya eneo hilo "kutokuwepo na kituo chochote cha afya", huku kituo cha karibu kikiwa zaidi ya kilomita 200 kutoka sehemu hiyo.

Mwezi Mei hospitali ya MSF katika eneo la Old Fangak kaskazini mwa Sudan Kusini ilishambuliwa kwa bomu, kuharibu sehemu yake ya dawa na shehena yote ya dawa.

Tukio hilo limekuja baada ya jeshi kutishia kushambulia eneo hilo kutokana na ‘‘kuvamia’’ maboti ambapo wanalaumu washirika wa Machar kufanya hivyo.

Sudan Kusini imekumbwa na hali tete ya usalama tangu kupata uhuru kutoka kwa Sudan 2011.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us