Kitenge, asili yake sio Afrika
Kitenge, asili yake sio Afrika
Historia inaonyesha kitenge kimeletwa na Waholanzi na asili yake ni kutoka nchini Indonesia.
28 Machi 2025


Kuwa na nguo ya kitenge siku hizi imekuwa ni jambo la kawaida. Inaweza kuwa ni katika mfumo wa nguo, kinyasa, suruali, shati au koti.

Mbali na hivyo, matumizi ya vitenge pia yameongezeka, na kutumiwa katika mapambo ya viti na hata mapazia. Hii ni dhahiri kwamba, kitenge kinazidi kupata umaarufu, na mtu akivaa kitenge anaonekana mtanashati. 

Hata hivyo, unajua kuwa kitenge asili yake sio Afrika? 

Historia inaonyesha kitenge kimeletwa na Waholanzi na asili yake ni kutoka nchini Indonesia. 

Simulizi pia inaonyesha kuwa katika karne ya 19 wakoloni wa Uholanzi wakiwa Indonesia walivutiwa na miundo ya batiki iliyoundwa na mafundi wa Javanese, kabila kubwa nchini Indonesia. 

Waholazi wakataka kufanya biashara, hivyo wakazalisha kwa wingi viwandani wakilenga soko la ndani la Indonesia. Hata hivyo, watu wa Indonesia walipendelea zaidi batiki zao za kitamaduni zilizotengenezwa kwa mikono.

Na hapo Waholanzi wakalazimika kutafuta soko la nje. Wakati nchi za ulaya zilikuwa zikigawana Afrika Mashariki kwa ajili ya ukoloni miaka ya 1885, Uholanzii ilikuza mauzo yake ya kitambaa hicho katika maeneo haya, na hapo kitenge kikafika Afrika mashariki.

Ukifika nchi za Afrika Magharibi, utakiita kitambaa cha Ankara. Hapa inaripotiwa kililetwa na wanajeshi wa Afrika magharibi ambao walikuwa wakihudumu nchini Indonesia, ambao walirudi nyumbani na vitambaa vya batiki kama zawadi.

Kwa haraka vikapata maarufu na wenyeji wakaanza kubadilisha chapa na kuunda miundo tofauti ya kitambaa wakiwa na mchanganyiko wa rangi, miundo, na alama zilizokuwa na ladha ya Kiafrika.

Kitenge pia kinaitwa chitenge au zitenge katika nchi nyengine, ikiwa pia kinavaliwa sana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ingawa zamani vazi la kitenge lilihusishwa na wazee, lakini hivi mambo yamebadilika.

Ubunifu katika sekta ya mitindo umekipa kitenge muonekano mpya na wa kisasa, hasa baada ya ubunifu wa mishono ya kisasa. Pia kuna wale wanaoamini kuwa ukinunua kitenge DRC na upate fundi Mkongo, basi una uhakika wa kutapata vazi la kipekee.

Hii ni kwa sababu, kitenge kinavaliwa sana nchini DRC katika mishono tofauti na ya kipekee inayopendeza.

Makampuni ya kimataifa pia yanatumia kitenge kushona nguo zao kwa kufuata mitindo ya kisasa, huku wasanaii maarufu wa kimataifa nao wanavaa nguo zilizotengezwa na vitenge.Barani Afrika kitambaa hiki si kwa ajili ya mitindo ya nguo tu, ila kimekuwa ishara ya utambulisho na urithi wa kiafrika.

Rangi na miundo tofauti ya kitambaa inabeba maana tofauti.

Kuna vile zinavyovaliwa katika sherehe kama harusi, na kuna ambavyo vimetengwa kwa ajili ya matukio maalumu kama misiba.

Yaani kitenge  barani Afrika, sasa hivi sio tena kitambaa kilichopitwa na wakati, urembo wake utategemea ile mshono ambayo fundi wako atakutengenezea.
Bila shaka, hata wewe katika msimu huu wa sherehe utakuwa na nguo yako ya kitenge.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us