Munyakho, ambaye kwa sasa anajulikana kwa jina la Abdulkareem, alifungwa jela katika gereza la Shimeisi mjini Makkah na aliachiliwa siku ya Jumanne saa nne asubuhi.
“Ubalozi wetu mjini Riyadh umethibitisha kuwa Steve amefanya ibada ya Umra (hija ndogo) pindi alipoachiliwa,” Katibu Mkuu aliandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne.
Umrah ni ibada ya hija ndogo ya kwenda Makkah, mji mtakatifu wa Waislamu, ambayo inaweza kutekelezwa wakati wowote, tofauti na Ḥajj, ambayo wakati wake ni maalum.
“Tutatoa taarifa kamili kuhusu lini atawasili nchini. Nawapongeza wote wale waliotuunga mkono katika juhudi za kusaidia kuachiliwa kwake huru,” King’oei aliongeza.
Munyakho alikuwa anafanya kazi nchini Saudi Arabia kama meneja wa bohari na alihukumiwa kuuawa kwa upanga baada ya kupigana na mwenzake raia wa Yemen Aprili 2011. Baadaye raia huyo wa Yemen alifariki kutokana na majeraha.
Mwezi Machi, Katibu Mkuu wa chama tawala cha UDA nchini Kenya Hassan Omar alitangaza kuwa serikali za Saudia Arabia na Kenya zilifikia makubaliano ya malipo ya fidia ya dola za Marekani milioni 1.